Polisi wa Burundi kuondolewa Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9019-polisi_wa_burundi_kuondolewa_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya kuondolewa maafisa wa polisi wa Burundi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao wa Julai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2016 00:00 UTC
  • Polisi wa Burundi kuondolewa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya kuondolewa maafisa wa polisi wa Burundi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao wa Julai.

Umoja huo umetoa taarifa na kusema kuwa, maafisa wa polisi wa Burundi wanaoshiriki katika operesheni za kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati wataondolewa mjini Bangui tarehe 31 Julai, 2016.

Hata hivyo Umoja wa Mataifa haukutoa maelezo zaidi kuhusiana na uamuzi huo.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, askari hao wa Burundi hawatabadilishwa na askari wa nchi nyingine yoyote wakati watakapoondolewa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Burundi ina maafisa 280 wa polisi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui.

Kwa upande wake mshauri mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko CAR hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa kutokana na kuongezeka tuhuma za uvunjaji wa haki za binadamu na ukandamizaji nchini Burundi.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2014 Burundi ilituma wanajeshi 12 elfu wa kulinda amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.