Jun 29, 2023 02:52 UTC
  • Baraza la Usalama latakiwa kushughulia jinai dhidi ya raia katika mapigano ya Sudan

Asasi na jumuiya 41 zenye mfungamano na wanawake Afrika, zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatilia na kushughulikia jinai dhidi ya raia nchini Sudan zinazofanywa na pande mbili hasimu katika vita vyao.

Taarifa ya asasi na jumuiya hizo inataka kushinikizwa pande mbili hasimu nchini Sudan ili zikomeshe jinai dhidi ya raia sambamba na kufungua njia kwa ajili ya kufikishwa misaada ya kibinadamu.

Sehemu nyingine ya takwa hilo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imezituhumu pande mbili hasimu nchini Sudan kwa kutenda jinai dhidi ya raia.

Sudan ilikumbwa na mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na askari wa kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) wanaoongozwa na Kamanda Muhammad Hamdan Dagalo kuanzia Aprili mwaka huu. Mapigano hayo yamekuwa yakijiri katika mji mkuu Khartoum na katika miji mingine ya kaskazini na magharibi mwa nchi. 

Mapatano ya kusimamisha mapigano yametangazwa kwa mara kadhaa huko Sudan hadi sasa hata hivyo pande zinazopigana zimekuwa zikikiuka mapatano hayo mara kwa mara. 

Haitham Ibrahim, Waziri wa Afya wa Sudan, ametangaza kwamba hadi sasa mapigano hayo ya ndani yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000 na kujeruhiwa wengine 6,000.

Umoja wa Mataifa umegusia juu ya uwezekano wa kushuhudiwa jinai dhidi ya binadamu huko Darfur na kutahadharisha kuwa mzozo unaoendelea jimboni humo umechukua mwelekeo wa kikabila katika eneo hilo. 

Tags