Chama kimoja cha siasa Malawi chataka UN kuchunguza ajali ya ndege iliyomuua Makamu wa Rais
(last modified Fri, 14 Jun 2024 11:25:08 GMT )
Jun 14, 2024 11:25 UTC
  • Chama kimoja cha siasa Malawi chataka UN kuchunguza ajali ya ndege iliyomuua Makamu wa Rais

Chama cha siasa cha Malawi Alliance for Democracy kimemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kikiuomba umoja huo kuingilia kati uchunguzi kuhusu ajali ya ndege iliyotokea Jumatatu na kumuua Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima na wengine wanane.

Chama hicho ni miongoni mwa vyama tisa vya muungano vilivyoendesha kampeni hadi kumuwezesha Rais wa Malawi Lazarus Chakwera kuingia madarakani katika uchaguzi wa kihistoria wa marudio wa mwaka 2020.

Barua hiyo, iliyoandikwa jana Alkhamisi na kutiwa saini na mwenyekiti wa chama hicho Enoch Chihana, imesema kwamba chama hicho kinachukulia janga hilo kama suala la kitaifa kwa kuwa linahusisha mtu muhimu mno kisiasa, hivyo msaada wa Umoja wa Mataifa ni muhimu.

Barua hiyo pia imetaka uungaji mkono wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Umoja wa Afrika katika uchunguzi wa ajali hiyo na kubainika uhalisia wa mambo.

Chama hicho kimeorodhesha mambo matatu ya kuzingatiwa katika uchunguzi huo, ikiwa ni pamoja na kutangazwa eneo la ajali ya ndege kama eneo la uhalifu.

Waziri wa Habari na Uwekaji Dijitali wa Malawi Moses Kunkuyu alisema Jumatano kwamba Jeshi la Ulinzi la Malawi na Huduma ya Polisi ya Malawi litachunguza ajali hiyo ingawa hali mbaya ya hewa iliripotiwa kuwa ndicho chanzo chake.

Rais Chakwera ametangaza siku 21 za maombolezo na ametoa wito wa utulivu na umoja miongoni mwa Wamalawi wote.

Tags