Mar 28, 2024 03:11 UTC
  • Rais wa Iran: Palestina sasa ni kadhia ya ulimwengu wa ubinadamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kutokana na muqawama au mapambano ya Kiislamu na misimamo imara ya wananchi wanaodhulumiwa na wenye nguvu wa Gaza, kadhia ya Palestina sasa imevuka mipaka ya ulimwengu wa Kiislamu na kuwa suala la ulimwengu wa ubinadamu.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatano alikutana na Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kumpongeza kwa mnasaba wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na ushindi na hamasa kubwa ya watu wa Gaza katika kusambaratisha malengo ya utawala ghasibu wa Israel. Ameongeza kuwa, watu wa dunia wanauchukia utawala dhalimu wa Israel na muungaji mkono wake mkuu, Marekani, huku wakiwa wanawapenda watu wanaodhulumiwa wa Gaza.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, harakati kubwa na ya kivita ya jeshi la wanamapambano wa Palestina katika operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqsa " ni tukio la kipekee ambalo limetoa kipigo kisichoweza kufidiwa kwa utawala wa Kizayuni. Amesema kwamba kile ambacho kimethibitishwa leo kwa watu wote duniani ni uhalali na kuwa katika haki kadhia ya ukombozi wa Palestina na watetezi wa kadhia hiyo ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kiislamu. Halikadhalika amesema dunia imeweza kubaini kuwa utawala utendao jinai wa Israel ndio chimbuko la ukosefu wa usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia na ni utawala unaopinga amani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdolahian akimkaribisa Ismail Haniya jijini Tehran Jumatatu 

Rais wa Iran aidha  amesema harakati zote  za kidiplomasia za Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo hilo ni hadaa tupu na kueleza kwamba leo hii nchi zilizoanzisha uhusiano wa kawaida utawala huo wa kihalifu zimefedheheshwa na kuaibishwa mbele ya watu wao. Ameongeza kuwa: Matukio ya hivi karibuni ya Gaza ni kashfa kubwa kwa Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi ambazo zinaunga mkono utawala wa Kizayuni unaoua watoto kiholela. Aidha amesema matukio ya Gaza kwa hakika yamefichua utambulisho halisi wa Marekani na Magharibi kwa mataifa ya dunia.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ameashiria pia juhudi kubwa za Iran za kuanzisha mshikamano baina ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Gaza huku akikosoa udhaifu wa wakuu wa baadhi ya nchi za Kiislamu katika kukabiliana na jinai za Israel dhidi ya Gaza.

Ismail Haniyah kwa upande wake amepongeza juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina. Amesema jitihada hizo zinazotokana na imani ya kidini ni matokeo ya mtazamo wa kina wa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags