Msomi wa Kisunni Iran atoa wito wa kuugwa mkono Waislamu Kashmir
Msomi wa Kisunni ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Wataalamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito kwa Waislamu kote duniani kulaani mauaji ya hivi karibuni ya ndugu zao wa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India.
Molavi Ahmad Salami amewataka Waislamu kuonyesha uungaji mkono wao kwa ndugu zao wa Kashmir na kusisitiza kuwa, kadhia ya eneo hilo linalodhibitiwa na India imeendelea kufumbiwa macho na ulimwengu wa Kiislamu kama kadhia ya Palestina. Msomi huyo wa Kisunni nchini Iran ameongeza kuwa, ni jukumu la kila Muislamu kusimama na kupinga dhulma na mateso wanayopitia Waislamu wa Kashmir. Amesisitiza kuwa, katika hali ambayo haifai kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, lakini wapenda haki duniani na haswa nchi za Kiislamu zina wajibu wa kuwaunga mkono kisiasa Waislamu wa Kashmir.
Haya yanajiri siku moja baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoa wito wa kuwepo utulivu baina ya pande hasimu katika eneo la Kashmir inayodhibitiwa na India. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassem alisema mzozo wa Kashmir unaweza kutatuliwa kwa njia za amani na mazungumzo.
Watu wasiopungua 45 wameuawa katika machafuko yaliyoanza Julai 9 katika eneo hilo huku wengine 3,500 wakijeruhiwa, baada ya jeshi la India kutumia nguvu kupita kiasi kuwakandamiza waandamanaji ambao wamekuwa wakitoa nara za kutaka uhuru.
Kashmir ni jimbo lenye Waislamu wengi India na limekuwa likikumbwa na mzozo tokea India ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947.