Iran kuanza kuziuzia nchi za Ulaya mapipa laki 8 ya mafuta kwa siku
(last modified Mon, 20 Mar 2017 08:02:21 GMT )
Mar 20, 2017 08:02 UTC
  • Iran kuanza kuziuzia nchi za Ulaya mapipa laki 8 ya mafuta kwa siku

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatazamiwa kuongeza kiwango cha mauzo yake ya mafuta kwa nchi za Umoja wa Ulaya EU.

Ali Kardor, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Mafuta la Iran NIOC amesema kuwa, Iran itaanza kuziuzia nchi za Ulaya mapipa laki nane ya mafuta kwa siku katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Kardor akisema hayo na kuongeza kuwa, kwa sasa kiwango cha mauzo ya mafuta ya Iran kwa nchi za EU ni mapipa laki 5 kwa siku.

Mapema mwezi huu, Sirous Kianersi, Meneja wa Shirika la Taifa la Meli za Mafuta la Iran alisema kuwa, meli za mafuta za Jamhuri ya Kiislamu zimerejea kwenye bandari za barani Ulaya.

Ali Kardor, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Mafuta la Iran NIOC

Alisisitiza kuwa, hayo ni miongoni mwa mafanikio ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kwamba, baada ya kuanza kutekelezwa makublianao hayo na kuondolewa vikwazo, safari za meli za mafuta za Iran kuelekea Ulaya zimeanza tena baada ya kuzuiwa wakati wa vikwazo.

Licha ya kuimarika soko la mafuta la Iran katika nchi za Ulaya na hata kupata wateja wapya kama Hungary baada ya kuanza kutekelezwa makubalioano ya nyuklia ya Vienna, lakini Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikiuza kiwango kikubwa zaidi cha mafuta ghafi kwa nchi za bara Asia kama vile India, Korea Kusini, China na Japan.

Tags