Madaktari Wairani kuwatibu Wairaqi waliohujumiwa na ISIS
Timu ya madaktari wa Iran wameelekea Iraq kuwasaidia waathirika wa hivi karibuni wa hujuma ya silaha za sumu zilizotumiwa na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika mkoa wa Kirkuk.
Waziri wa Afya wa Iran Hassan Qadhizadeh Heshemi amesema madaktari hao wametumwa Iraq kufuatia ombi la dharura la nchi hiyo ya Kiarabu.
Ameongeza kuwa madaktari hao watachunguza hali ya majeruhi na kuwapa dawa na huduma za dharura za kitiba.
Siku ya Jumatano Waziri wa Afya wa Iraq Adilah Husayn alimpigia simu mwenzake wa Iran na kuomba msaada wa dharura kuwasaidia waliojeruhiwa katika hujuma ya silaha za kemikali iliyotekelzwa na magaidi wakufurishaji wa ISIS huko Kirkuk. Binti wa miaka mitatu alipoteza maisha na watu wengine zaidi ya 600 kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya kinyama ya Daesh.
Hujuma hiyo ilijiri Jumamosi asubuhi katika mji wa Taza ambao pia ulishambuliwa kwa maroketi yaliyokuwa na kemikali siku tatu kabla ya tukio hilo.