Rais Rouhani: Marekani imetengwa kwa hatua yake ya kuvuruga mapatano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35755-rais_rouhani_marekani_imetengwa_kwa_hatua_yake_ya_kuvuruga_mapatano_ya_nyuklia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kubakia Marekani peke yake kufuatia hatua yake ya kuvuruga mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA ni kati ya mafanikio ya Iran
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2017 02:40 UTC
  • Rais Rouhani: Marekani imetengwa kwa hatua yake ya kuvuruga mapatano ya nyuklia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kubakia Marekani peke yake kufuatia hatua yake ya kuvuruga mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA ni kati ya mafanikio ya Iran

Rais Rouhani ameyasema hayo Jumatatu mjini Tehran wakati alipokutana na wawakilishi wa Jumuiya ya Wanazuoni Wanamapambano na kuongeza kuwa, JCPOA ni mapatano yenye thamani ambayo yanatokana na kauli moja ya kitaifa, uungaji mkono wa wananchi na muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Rouhani ameendelea kuashiria kuhusu fursa zilizojitokeza kufuatia mapatano hayao kama vile kuondolewa vikwazo, kutatuliwa hatua kwa hatua matatizo ya kibenki na ongezeko la uwekezaji wa kigeni na kuongeza kuwa: "Kwa mtazamo wa kisiasa, kubakia peke yake Marekani kutokana na hatua yake ya  kuvuruga mapatano ya JCPOA na kuwepo kauli moja ya jamii ya kimataifa katika kuunga mkono mapatano hayo ni kati ya mafanikio makubwa ya Iran."

Baada ya Rais wa Marekani kutangaza kupinga mapatano hayo ya JCPOA siku ya Ijumaa, nchi zingine zilizoyatia saini yaani Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya zimetangaza kuyaunga mkono huku zikisisitiza kuwa Iran imetekekeza ahadi zake katika mapatano hayo ya nyuklia.

Kwingineko katika matamshi yake, Rais Hassan Rouhani amesema, Uislamu  na mfumo wa jamhuri ni nguzo muhimu za mfumo wa Kiislamu wa Iran na ni turathi zenye thamani za Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Rouhani amesisitiza kuwa, serikali ya Iran imetokana na irada ya taifa na wakati huo huo inatekeleza mafundisho ya Kiislamu.