Zarif: Trump anadunisha demokrasia kwa kutishia wapinzani wake
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa vikali msimamo wa Marekani wa kupinga maamuzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Quds tukufu na kusema kuwa: Washington imebakia katika kiwango cha "ama uwe pamoja na sisi au dhidi yetu."
Muhammad Javad Zarif amesema kuwa, kwa kutoa vitisho dhidi ya wale wote wanaofanya ujasiri wa kupinga matakwa yake ya kidhalimu, Rais Donald Trump wa Marekani ameonesha kuwa anadunisha na kudhalilisha demokrasia katika upeo wa dunia.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza hayo baada ya Donald Trump kutoa vitisho dhidi ya nchi zilizopinga uamuzi wa Marekani wa kuitambua Quds tukufu (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel kinyume kabisa na maazimio ya Baraza la Usalama.
Mapema jana Rais wa Marekani alisema kuwa, Washington itakata misaada ya kifedha kwa nchi zilizopigia kura dhidi ya uamuzi wake wa kuitambua Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel.
Nchi za Kiislamu na Kiarabu zimetoa wito wa kuitishwa kikao cha dharura cha nchi 193 wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kujadili uamuzi wa Trump kuhusu Quds tukufu. Wito huo umetolewa siku kadhaa baada ya Marekani kutumia kura ya veto kwa ajili ya kukwamisha azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa likipinga na kulaani uamuzi wa Trump wa kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.