Iran haifanyi mazungumzo tena kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Fri, 16 Mar 2018 06:50:48 GMT )
Mar 16, 2018 06:50 UTC
  • Iran haifanyi mazungumzo tena kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa katu haitakubali kufanyika mazungumzo mapya kuhusu mapatano ya nyuklia baina yake na mdola sita makubwa duniani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi akizungumza Alhamisi kufuatia jitihada za Marekani za kutaka kubadilisha mapatano hayo ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekeelzwaji, JCPOA, amesema mapatano hayo ni ya kimataifa na hayawezi kujadiliwa upya.

Araqchi ambaye yuko Vienna, Austria kushiriki katika Kikao cha Tume ya Pamoja ya JCPOA ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hakuna uwezekano wa kuongezwa ibara mpya n.k katika mapatano hayo ya nyuklia. Kikao hicho cha Tume ya Pamoja ya JCPOA kinatazamiwa kufanyika leo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umechapisha ripoti 10 ambazo zote zimebaini kuwa, Iran imeheshimu kikamilifu majukumu yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Kwa msingi huo amesema pande zote zinapaswa kutekeleza majukumuu yao katika mapatano hayo.

Itakumbukwa kuwa Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilifikia mapatano kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran. Mapatano hayo ambayo ni maarufu kama JCPOA kwa kifupi yalifikiwa Julai 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 16 mwaka 2016. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia huku nchi za Magharibi zikitakiwa ziiondolee Iran vikwazo. Lakini pamoja na hayo Marekani inakaidi mapatano hayo huku Rais  Donald Trump wa nchi hiyo akitishia kuiondoa nchi yake katika JCPOA.

Tags