Bahram Qassemi: Iran itatoa majibu dhidi ya vitendo vya kiuadui dhidi yake
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran itachukua hatua ya lazima na mwafaka mkabala na kitendo chochote kile cha kiuadui ambacho kitakuwa dhidi ya maslahi ya kitaifa ya Iran.
Bahram Qassemi amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mkutano wake na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi akijibu misimamo ya Marekani na Ufaransa kuhusiana na hatua ya Iran katika masuala ya anga na kutuma angani satalaiti angani. Amesema kuwa, shughuli za Iran hazikinzani na azimio lolote lile la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama likiwemo azimio nambari 2231.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia misimamo mikali ya baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Iran na kuchelewa kwa miezi kadhaa uanzishwaji wa mfumo wa mabadilishano ya fedha baina ya Iran na Ulaya kwa kifupi SPV baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema kuwa, madola ya Ulaya yana matumaini kwamba, iwe ni kwa haraka au kwa kuchelewa, yatafanikisha mfumo huo na kuna ishara zinazoonyesha kwamba, madola hayo yana nia ya kutekeleza mpango huo.
Bahram Qassemi amezungumzia pia siasa za Marekani katika Mashariki ya Kati na mpango wa Washington wa kuondoa wanajeshi wake nchini Syria na kusema kuwa, sera kuu za Marekani ni kubomoa miundombinu ya nchi za Kiislamu.