Iran yazilaumu nchi zinazounga mkono vikwazo vya Marekani dhidi yake
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya sheria na ya kimataifa amesema kuwa nchi ambazo zinaunga mkono vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa la Iran zinavunja roho ya mshikamano kati ya Waislamu.
Gholamhossein Dehghani amesema hayo katika kikao cha 46 cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Abu Dhabi, Imarati na huku akielezea kusikitishwa kwake na vipaumbele visivyo sahihi vinavyotolewa na jumuiya hiyo amesema kuwa, kuna idadi ndogo ya wanachama wa OIC wanatumia fedha nyingi kujaribu kuigeuza jumuiya hiyo kuwa chombo cha kufanikishia siasa zao za kigeni suala ambalo kwa hakika linazidi kuipotezea heshima na itibari OIC.
Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitizia wajibu wa kuendelea kupewa kipaumbele cha kwanza kadhia ya Palestina na kuongeza kuwa, Tehran haitoruhusu jambo lolote lile linalohusu ulimwengu wa Kiislamu liharibu suala kuu na la muda mrefu zaidi la ulimwengu huo nayo ni kadhia ya Palestina.
Amegusia pia hatua ya Marekani ya kuuhamishia Quds ubalozi wake uliokuweko Tel Aviv na kukumbusha kwamba, hiyo ni moja ya njama za Marekani inayotekelezwa kwa jina la "Muamala wa Karne." Amesema, baadhi ya wanachama wa OIC wameidharau hatua hiyo ya Marekani na hivi sasa wanajaribu kuzipotosha fikra za walio wengi katika ulimwengu wa Kiislamu na kuzisahaulisha kadhia yao kuu na muhimu zaidi ya kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina.
Kikako cha 46 cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa OIC kilianza juzi Ijumaa mjini Abu Dhabi kwa uenyekiti wa waziri wa mambo ya nje wa Imarati, Abdullah bin Zayed Aal Nahyan.