Mwakilishi wa Iran UN: Marekani imekiuka mkataba wa NPT
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametilia mkazo jukumu la pamoja la kupiga marufuku aina yoyote ya majaribio ya uripuaji silaha za nyuklia na kueleza kwamba Marekani imekiuka mkataba wa kuzuia uundaji na uenezaji silaha za nyuklia (NPT) kwa kujitoa kwenye makubaliano yanayohusiana na mkataba huo na kwa kuanzisha mashindano ya kuzifanya silaha hizo za nyuklia kuwa za kisasa zaidi.
Majid Takht Ravanchi ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa anuani ya "Siku ya Kupinga Majaribio ya Nyuklia" na kubainisha kuwa, mashindano mapya ya silaha na mashindano ya kuzifanya silaha za atomiki kuwa za kisasa zaidi yanatia wasiwasi. Amefafanua kuwa, katika zama ambapo baadhi ya nchi zenye silaha za atomiki zina mipango mbali mbali ya kustawisha silaha hizo na kuweza kuzitumia kwa njia rahisi zaidi, suala la kukomesha majaribio ya miripuko ya silaha za nyuklia linazidi kuwa na umuhimu.

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa miripuko ya aina yoyote ya nyuklia inapasa ipigwe marufuku kikamilifu na akaongezea kwa kusema: Kwa mujibu wa ripoti za karibuni, Marekani si tu haina nia ya kupitisha mkataba kamili wa kupiga marufuku majaribio ya atomiki lakini inaanzisha majaribio ya miripuko ya atomiki ikiwemo majaribio ya kuripua silaha za atomiki za chini ya ardhi.
Takht Ravanchi amebainisha kuwa: Sera zisizo na nadhari wala uwajibikaji za Marekani, ya karibuni kabisa ikiwa ni kujitoa nchi hiyo katika mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF) zina madhara kwa jitihada zote zinazofanywa kimataifa kwa ajili ya kuangamiza silaha za atomiki na kuzuia uenezaji wake na inapasa sera hizo za Washington zikomeshwe.../