Marais wa Iran na Ufaransa wajadili suala la kuondolewa vikwazo Tehran
Rais wa Iran amesisitiza juu ya udharura wa kuondolewa vikwazo wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu, katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Ufaransa.
Sayyid Ebrahim Raisi amemwambia Emmanuel Macron kuwa, sanjari na kuondolewa vikwazo, lakini taifa la Iran linataka kupewa dhamana ya kivitendo ya kufutwa vikwazo hivyo, na vile vile hakikisho la utekelezaji faafu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Rais wa Iran huku akiashiria kukiri Marekani kufeli kwa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya taifa la Iran amebainisha kuwa, Tehran tayari imeonyesha kivitendo azma na irada ya kufikiwa makubaliano mwishoni mwa mazungumzo ya kujaribu kuhuisha JCPOA yanayofanyika huko Vienna.
Aidha katika mazungumzo hayo ya simu ya jana usiku, Marais wa Iran na Ufaransa wamejadili njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili baina ya Tehran na Paris.
Sayyid Raisi mbali na kulaani mashambulio dhidi ya wananchi wa Yemen amesisitiza kuwa, usalama na uthabiti katika eneo la Asia Maghairibi utapatikana tu kwa suluhu ya kieneo bila uingiliaji wa madola ajinabi, huku akiiasa jamii ya kimataifa itilie maanani mgogoro wa kibinadamu unaolikabili taifa maskini la Yemen.
Kwa upande wake, Rais wa Ufaransa amesema Iran ina haki ya kutoiamini Marekani, kwa kuwa mgogoro unaoshuhudiwa hivi sasa ulisababishwa na mienendo ya Wamarekani. Kadhalika amelaani mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen, hususan hujuma za anga za hivi karibuni dhidi ya wananchi wasio na hatia wa nchi hiyo ya Kiarabu.