Iran: Shabaha yetu ni kufikia mapatano mazuri katika mazungumzo ya Vienna
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, licha ya njama kubwa zilizofanywa na serikali ya Trump huko Marekani lakini njama zake zote zilishindwa mbele ya Iran na hakuweza kulipigisha magoti taifa hili wala kulifanya litengwe. Amesema, shabaha ya Tehran ni kufikia mapatano mazuri katika mazungumzo ya Vienna, Austria.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hossein Amir-Abdolahian amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya Euro News usiku wa kuamkia leo Jumatano na kuongeza kuwa, kitendo cha rais wa Marekani Joe Biden cha kuendelea kuiwekea vikwazo Iran hakiendani hata kidogo na madai yake kuwa ana nia njema na anataka kufikiwe makubaliano mazuri katika mazungumzo ya Vienna.
Hivi sasa mazungumzo yanaendelea mjini Vienna Austria, baina ya Iran na kundi la 4+1 linaloundwa na nchi za Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Russia na China kwa uratibu wa Umoja wa Ulaya.
Awamu hii ya nane ya mazungumzo ya Vienna kwa ajili ya kuondolewa Iran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa, imepiga hatua nzuri kutokana na ubunifu wa Tehran. Hata hivyo kasi ya mazungumzo hayo si ile inayotakiwa kutokana na uzoroteshaji unaofanywa na nchi za Magharibi hasa serikali ya Joe Biden na matatizo yaliyosababishwa na serikali iliyopita ya Marekani kwenye mapatano ya JCPOA.
Muda wote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, kwa vile Marekani ndiyo iliyojitoa yenyewe kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kwa vile ndiyo iliyoiwekea vikwazo Tehran bila ya sababu yoyote, ni Washington ndiyo inayopaswa kuondoa vikwazo hivyo na kutekeleza ahadi zake ndani ya JCPOA.