IRGC: Israel italipa gharama ya kuua shahidi Wairani wawili huko Syria
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema hakuna shaka utawala wa Kizayuni wa Israel utalipa gharama kubwa kwa jinai yake ya kutekeleza shambulizi lililopelekea kuuawa shahidi askari wawili wa SEPAH nchini Syria.
Taarifa ya Ofisi ya Uhusiano Mwema ya IRGC imeeleza kuwa, shambulizi la kombora la utawala haramu wa Israel viungani mwa mji mkuu wa Syria, Damascus juzi Jumatatu liliua shahidi mashujaa wawili wa jeshi hilo, ambao ni Kanali Ehsan Karbalaeepour na Kanali Morteza Saeednejad.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limesisitiza kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa litalipiza kisasi kwa jinai hiyo iliyofanywa na Wazayuni maghasibu.
Hii si mara ya kwanza kwa utawala huo khabithi kufanya hujuma dhidi ya washauri wa kijeshi wa Kiirani, ambao wako nchini Syria kwa mwaliko rasmi wa Rais halali wa nchi hiyo, Bashar al-Assad.
Mwaka 2018, wanajeshi wa utawala huo pandikizi waliwaua shahidi washauri kadhaa wa kijeshi wa Iran katika shambulizi jingine lililolenga kambi ya jeshi ya T-4 katika mji wa Homs, magharibi mwa Syria.
Syria imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo mara kadhaa ikitaka kusimamishwa haraka iwezekanavyo mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni.