Jan 29, 2023 13:22 UTC
  • Spika wa Bunge la Algeria: Tunataka kuimarisha uhusiano na Iran

Spika wa Bunge la Algeria amesema: Tunajivunia mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga mbalimbali na tunataka kuimarisha uhusiano kati ya mataifa yetu mawili.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) na ujumbe aliofuatana nao, wameelekea nchini Algeria kushiriki mkutano wa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
 
Katika mazungumzo yaliyofanyika leo kati ya maspika wa mabunge ya nchi mbili pembeni ya mkutano wa 17 wa mabunge ya nchi wanachama wa OIC, Ebrahim Boughali, Spika wa Bunge la Algeria amesema: "tunataka kuimarishwa uhusiano kati ya nchi mbili."
 
Boghali ameendelea kueleza kuwa, piganio tukufu la Palestina ni suala kuu na muhimu na akaongeza kuwa: Algeria inafanya juhudi ili nchi ya Palestina iweze kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.
 
Spika wa Bunge la Algeria ameeleza kwamba, hujuma zote dhidi ya Uislamu na kuchomwa moto Qur'ani hivi karibuni vinaonyesha kuwa Uislamu ndio ukweli na haki, na akasema: "tunakabiliana na changamoto kama hizi, na changamoto hizi zinatupa Waislamu sote jukumu la kuionesha kwa uzito mkubwa sura na taswira sahihi ya Uislamu.
 
Katika mazungumzo hayo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kufurahishwa na kuwepo kwake nchini Algeria na akasema: "viongozi na wananchi wa Iran wana mtazamo chanya na wa karibu kuhusiana na wananchi wa Algeria na viongozi wa nchi hii".

Qalibaf aidha amesema: "tunatumai kuwa kustawishwa uhusiano kati ya nchi mbili, kwa upande wa serikali na kwa upande wa mabunge, kutawezesha kustawishwa uhusiano katika nyanja za kiuchumi na kiutamaduni, na pia kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na kufanikisha mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina".

 
Spika wa Bunge la Iran ameongezea kwa kusema: "siku hizi serikali za Magharibi zimekuwa zikieneza chuki dhidi ya Uislamu na kuwapiga vita Waislamu; na wamewatusi Waislamu wote kwa kuichoma moto Qur'ani. Vilevile mashinikizo ya baraza jipya la mawaziri la utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina yameongezeka, lakini Wapalestina nao wametoa funzo kubwa kwa wazayuni".
 
Huku akisisitiza kuwa, bila ya shaka suala la Palestina ni suala la kwanza kwa Ulimwengu wa Kiislamu, Qalibaf ameongeza kuwa: "inatupasa nchi za Kiislamu tuelewe kuwa utawala wa Kizayuni unalenga kuliondoa suala la Palestina katika ajenda za Ulimwengu wa Kiislamu". 
Aidha amebainisha kuwa, Wazayuni wanataka kuvuruga umoja baina ya nchi za Kiislamu na kuvunja mwiko wa nchi za Kiislamu kutoanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni.
 
Qalibaf ameongeza kuwa: Serikali na umma wa Kiislamu inapasa zichukue hatua madhubuti zaidi kwa namna itakayoifanya nchi yoyote ile ya Kiislamu isithubutu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni.../

 

Tags