Dec 23, 2023 11:59 UTC
  • Wanasiasa wataka kufunguliwa mashitaka Wafaransa waliojiunga na jeshi la Israel kuua raia Gaza

Katika kashfa mpya ambayo inaendelea kutikisa misingi ya jamii ya Ufaransa na sambamba misimamo ya inayobadilika badilika ya serikali ya Paris kuhusu mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza, mbunge Thomas Portes wa chama cha "Fahari ya Ufaransa" amefichua uwepo wa Wafaransa 4,185 katika safu za jeshi la Israel linaloendelea kuua raia wa Palestina hususan wanawake na watoto wa Gaza.

Ingawa suala la kusajiliwa Wafaransa wenye uraia pacha katika jeshi la Israel ni jambo lililothibitishwa kwa miaka kadhaa, inaripotiwa kuwa katika vita vya sasa vya Gaza Wafaransa wanaunda kitengo cha pili cha wanajeshi wa kigeni baada ya Marekani.

Kujiunga kwa idadi hiyo kubwa ya Wafaransa katika jeshi la Israel linaloua raia wa Gaza kumewafanya wanasiasa na taasisi nyingi za kutetea haki za binadamu kutaka wafikishwe mbele ya sheria nchini Ufaransa, kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Palestina.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na idhaa ya Ufaransa ya "Europe 1", mbunge Portes amechapisha taarifa kwenye vyombo vya habari akiomba serikali ya Paris kuwafungulia mashtaka Wafaransa wanaoshiriki katika vita dhidi ya Gaza. Mbunge huyo wa eneo la Seine-Saint-Denis amesema, "Kama mbunge wa Ufaransa, siwezi kukaa kimya, na Ufaransa haiwezi kunyamaza kimya mbele ya jambo hili."

Jumatano iliyopita mbunge huyo alituma barua Waziri wa Sheria wa Ufaransa, Eric Dupont-Moretti, akimuomba atumie mamlaka yake kuanzisha uchunguzi dhidi ya maelfu ya Wafaransa wanaopigana Ukanda wa Gaza kwa niaba ya jeshi la utawala ghasibu na vamizi la Israel.

Amesema iwapo serikali haitachukua hatua atawasilisha ripoti kwa Mwendesha Mashtaka wa Umma mjini Paris kupitia Kifungu cha 40, na kutoa changamoto kwa serikali hadharani katikka kikao kijacho cha Bunge, kutokana na uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi la Israel, iwe Gaza au Ukingo wa Magharibi huko Palestina.

Kuhusu uwezekano wa kuhusika Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa katika kusafirisha maelfu ya vijana wa nchi hiyo kwenda kupigana vita huko Gaza kwa niaba ya utawala haramu wa Israel, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Shirika la Haki za Kibinadamu la AFDI, wakili Abdel Majeed Marari, anasema: Njia ya wazi inayotumiwa vijana wa Ufaransa kwenda kupigana huko Gaza baada ya Oktoba 7 inaonyesha kuwa serikali imebariki kitendo hicho na kuwapa mwanga wa kijani.

Wapalestina wasiopungua elfu 20 wameuawa hadi sasa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza na wengi wao ni wanawake na watoto. 

Tags