Feb 14, 2024 07:34 UTC
  • Nasrullah: Chimbuko la nguvu za muqawama ni Mapinduzi ya Kiislamu

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amelipongeza na kulishukuru Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kwa kuiunga mkono kambi ya muqawama katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sayyid Hassan Nasrullah katika hotuba aliyoitoa jana Jumanne kwa mnasaba wa Siku ya Maveterani alieleza kuwa, "Tangu mwanzo, IRGC imekuwa muungaji mkono halisi na wa kweli wa makundi ya muqawama."

Sanjari na kuipongeza Iran kwa maadhimisho ya miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sayyid Nasrullah amesema: Nguvu za mrengo wa muqawama hii leo zimetokana na Mapinduzi ya Kiislamu."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameashiria kusimama kidete Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya madola dhalimu na ya kibeberu na kutokubali kuburuzwa na kusisitiza kwamba, Iran ni mbeba bendera ya muqawama mkabala wa madhalimu.

Hizbullah usiku wa kuamkia leo imeshambulia kwa makombora kambi ya jeshi la Israel ya Zebedin, kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Kadhalika Sayyid Nasrullah amesema hakuna shaka kuwa adui Mzayuni atashindwa tu kutokana na kusimama kidete kwa wananchi wanamuqawama wa Palestina wakiungwa mkono na makundi yote ya muqawama katika eneo.

Amesema iwapo utawala wa Kizayuni utashadidisha uvamizi na mashambulizi yake katika eneo, hakuna shaka kuwa wanajihadi wa Hizbullah pia wataendelea kujibu mapigo na kupanua zaidi operesheni zao dhidi ya Wazayuni.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema katika siku 130 zilizopita tangu kuanza kwa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo uliyoyakusudia kwa kuuvamia na kuushambulia Ukanda wa Gaza.

Tags