Feb 28, 2024 11:50 UTC
  • Amir wa Qatar asisitiza ulazima wa kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni Ukanda wa Gaza

Amir wa Qatar amesisitiza kuwa kuna ulazima wa kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa  Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani jana alikuwa na mazungumzo huko Paris Ufaransa na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ambapo alisisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza. Sheikh Tamim alisema kuwa ulimwengu unashuhudia mauaji ya kimbari ya Wapalestina kupitia kuwasababishua njaa na kuwahamisha kwa lazima raia hao.

Mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya raia wa Gaza 

Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani pia ameeleza kuwa jamii ya kimataifa inaendelea kufeli katika kuwasaidia raia huko Ukanda wa Gaza na akaongeza kuwa: Tunapasa kukomesha mateso wanayopitia raia wa Palestina.  

Jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina zimechochea hisia za walimwengu; na katika maeneo yote ya dunia watu na serikali mbalimbali zimetoa wito wa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina. 

Utawala wa Kizayuni unaendesha mashambulizi makubwa ya kikatili katika maeneo ya Ukanda wa Gaza na  Ukingo wa Magharibi dhidi  ya raia wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina tangu Oktoba  7 mwaka jana hadi sasa kwa uungaji mkono wa pande zote wa nchi za Magharibi khususan Marekani.   

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Afya ya Palestina, takriban Wapalestina elfu 30 ambao wengi wao ni wanawake na watoto wameuawa shahidi tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Tags