CAIR: UN ichunguze jeshi la Israel lilivyowaua Wapalestina bila sababu na kuzifukia maiti zao
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani [CAIR] limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchunguza video inayoonyesha wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakiwapiga risasi bila sababuu Wapalestina wawili wanaoonekana kuwa hawana silaha kisha kuzifukia maiti zao kwa buldoza.
Picha za video zilizonaswa na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar zinaonyesha wanaume wawili wa Kipalestina wasio na silaha, mmoja akipunga hewani kipande cha kitambaa cheupe mara kwa mara kuashiria kujisalimisha, kabla ya askari katili wa jeshi la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuwapiga risasi na kisha kuzifukia maiti zao kwenye kifusi kwa kutumia tingatinga karibu na mji wa Ghaza.
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani vikali mauaji hayo, ikisema "ni ushahidi zaidi unaoonyesha ukubwa wa ufashisti, jinai na uhalifu unaotawala tabia na khulka ya Wazayuni".
Naye Profesa Richard Falk, ripota maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu huko Palestina amesema, ufyatuaji risasi huo uliofanywa na askari wa Kizayuni ni "uthibitisho wa wazi wa kuendelezwa ukatili wa Israel huko Ghaza" na ambao umekuwa ni kama "jambo la kila siku".../