Wapalestina: Gati ya muda inayotaka kujenga Marekani Ghaza ni "Bandari ya Uvamizi"
Wapalestina wanaielezea gati ya muda inayojengwa na Marekani kwenye pwani ya mji wa Ghaza kuwa ni "bandari ya uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu".
Mnamo tarehe 7 Machi, Rais Joe Biden wa Marekani alitangaza kwamba amelikabidhi jeshi la Marekani jukumu la kujenga gati ya muda karibu na Ghaza kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu inayohitajika sana, huku Israel ikiendelea kuruhusu chembe ndogo tu ya misaada kuingizwa katika eneo hilo kupitia nchi kavu.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ilitangaza kuwa ujenzi wa gati hiyo ya muda unaweza kuchukua hadi siku 60, na baada ya hapo milo milioni mbili kwa siku itaweza kutolewa kwa ajili ya Wapalestina Ghaza.
Maombi ya Wapalestina ya kupatiwa vifaa vya kuondoa vifusi vya nyumba zilizopigwa mabomu katika miezi kadhaa ya mashambulizi ya Israel, kuopoa miili ya marehemu, na kusaidia waliojeruhiwa hayajajibiwa kwa muda wote wa kipindi cha miezi sita iliyopita.
Hata hivyo, katika wiki za hivi karibuni, kwa msaada wa Marekani, mabuldoza na malori mengi yaliyotumwa na Israel kwenye mpaka wa Ghaza yamekuwa yakisafirisha maelfu ya tani za vifusi kutoka kwenye nyumba zilizobomolewa huko Ghaza vikiwa na viungo vya miili ya watu hadi kwenye pwanii ya eneo hilo ili kutumika katika ujenzi wa gati mpya.../