Dec 11, 2022 11:10 UTC
  • Wazayuni wawashambulia Wapalestina wakisherehekea ushindi wa Morocco

Jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel limewashambulia wananchi wa Palestina waliokuwa wamekusanyika kusherehekea ushindi wa Morocco katika mchuano wa robo fainali ya mechi za Kombe la Dunia zinazoendelea kushuhudiwa nchini Qatar.

Shirika la habari la Shahab limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, askari polisi na wanajeshi makatili wa utawala haramu wa Israel jana usiku waliwavamia na kuwashambulia Wapalestina katika eneo la Bab Al-Moud, walipokuwa wamejitokeza mabarabarani kufurahia ushindi wa Morocco.

Wananchi wa Wapalestina hiyo jana walijitokeza kwa wingi mabarabarani katika miji ya Quds, Alkhalil, Nablus, Qalqilya, Beitu Lahm (Bethlehem) na Gaza kusherehekea ushindi huo wa Morocco.

Timu ya taifa ya soka ya Morocco jana Jumamosi iliichabanga Ureno bao moja bila jibu, katika mchuano wa aina yake ya robo fainali ya Kombe la Dunia, uliopigwa katika Uwanja wa Al Thumama, yapata kilomita 12 kutoka Doha.

Bao hilo la pekee na la ushindi la Masimba wa Atlas lilifungwa na fowadi Youssef en-Nesyri, katika dakika ya 42 ya mchezo.

Mashabiki na wachezaji wa timu ya Morocco walisherehekea ushindi huo kwa kupeperusha bendera ya taifa linalokandamizwa na Israel la Palestina wakitangaza uungaji mkono wao kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu.

Palestina; Mshindi mkubwa zaidi katika Kombe la Dunia 2022

Vilevile wachezaji hao wa Morocco walionekana wakisujudu uwanjani wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio hayo.   Ushindi huo unaifanya Morocco kuwa timu ya kwanza ya Kiarabu na ya Kiafrika kufuzu kuingia raundi ya nusu fainali katika historia ya Kombe la Dunia. 

Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeipongeza Morocco kwa ushindi wa timu ya kandanda ya nchi hiyo dhidi ya Uureno hiyo jana na kufuzu kuingia nusu fainali.

Kabla ya hapo, Morocco iliishinda Uhispania kwa mabao matatu kwa bila katika mikwaju ya penalti katika mchujo wa kuwania kuingia robo fainali ya Kombe la Dunia.

Tags