Jihad Islami: Misimamo ya nchi za Kiarabu na Kiislamu ni dhaifu
Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetangaza kuwa misimamo dhaifu ya nchi za Kiarabu na Kiislamu inazidisha mateso na masaibu kwa watu wa Ghaza.
Tangu kuanza kwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa siku 17 zilizopita yaani tarehe 15 mwezi huu wa Oktoba, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makazi ya raia na maeneo ya umma kwa upande mmoja, kukatwa maji, umeme na uhaba mkubwa wa chakula na dawa kwa upande mwingine vimewasababishia hali mbaya sana raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Ghaza. Wakati huo huo taasisi za haki za binadamu zimetangaza kuwa, hali ya kibinadamu katika eneo hilo haielezeki na inasikitisha.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetoa taarifa na kutangaza kuwa: Misimamo ya nchi za Kiarabu na Kiislamu kuhusu Ghaza ni dhaifu na kwamba harakati za kisiasa za nchi mbalimbali mkabala wa Marekani na Magharibi zinatia shaka.
Taarifa ya Jihad Islami imesisiza kuwa: Kushindwa kutolewa misimamo rasmi mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kunazidisha mateso na matatizo kwa raia wa Ghaza wanaokabiliwa na vikwazo na mzingiro, na kwamba mapambano hayatashindwa mbele ya maghasibu, na istiqama ya wananchi wa Palestina itapelekea ushindi katika vita hivyo.
Wanamapambano wa Palestina Jumamosi tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba walianzisha oparesheni ya pande zote na ya aina yake iliyopewa jina la Kimbunga cha Al Aqsa kuanzia Ghaza (Kusini mwa Palestina) dhidi ya ngome na maeneo ya utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kutoa kipigo kikali cha utawala ghasibu wa Israel.