Kushadidi mashinikizo dhidi ya waungaji mkono wa Palestina nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i105918-kushadidi_mashinikizo_dhidi_ya_waungaji_mkono_wa_palestina_nchini_marekani
Marekani ikiwa ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni sio tu kwamba, imetoa uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kisilaha kwa utawala huo wakati wa vita vya Gaza, bali mfumo tawala wa Washington pia umeongeza mashinikizo dhidi ya waungaji mkono wa Wapalestina na wakosoaji wa jinai za utawala ghasibu wa Israel.
(last modified 2023-12-12T23:09:22+00:00 )
Dec 12, 2023 23:09 UTC
  • Kushadidi mashinikizo dhidi ya waungaji mkono wa Palestina nchini Marekani

Marekani ikiwa ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni sio tu kwamba, imetoa uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kisilaha kwa utawala huo wakati wa vita vya Gaza, bali mfumo tawala wa Washington pia umeongeza mashinikizo dhidi ya waungaji mkono wa Wapalestina na wakosoaji wa jinai za utawala ghasibu wa Israel.

Wafuasi wa Palestina, hasa katika vyuo vikuu, wanakabiliwa na kila aina ya mashinikizo na vitisho na mara kwa mara wako katika hatari ya kupoteza kazi au kulazimishwa kujiuzulu.

Katika suala hili, mnamo Desemba 5, Kamati ya Elimu na Nguvu Kazi ya Bunge la Marekani ilimwita Liz Magill Rais wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, Claudine Gay Rais wa Chuo Kikuu cha Harvard na Sally Kornbluth Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) ili kujibu maswali kuhusu hatua walizochukua kuhusuu maandamano dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza yaliyofanyika katika mazingira ya chuo. Hatua hii imechukuliwa na Congress ya Marekani baada ya kupitisha azimio la kulaani vitendo vya wanafunzi katika baadhi ya vyuo vikuu vya Marekani vya kutangaza uungaji mkono wao kwa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa azimio hilo, kuunga mkono Hamas, Hizbullah na makundi mengine ya muqawama katika taasisi za elimu ya juu za Marekani kulilaaniwa kwa madai kwamba, eti makundi hayo ni ya kigaidi. Licha ya kuwa, ilidaiwa katika azimio hilo tajwa kwamba, halina ulazima wa kisheria na kimsingi ni hatua ya kinembo tu, lakini kuitwa na kisha kusailiwa wakuu wa vyuo vikuu kadhaa vya Marekani ni jambo linalokwenda kinyume cha dai hili na wakati huo huo kuthibitisha kwamba, maudhui ya azimio hili yamo katika hali ya kutekelezwa katika vyuo vikuu vya Marekan.

 

Kufuatia hatua ya Bunge la Congress ya kumuita Liz Magill, Rais wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, ambaye aliitwa baada ya maandamano ya wafuasi wa watu wanaodhulumiwa wa Palestina kwenye ua wa chuo kikuu hiki na ambaye alikataa kulaani maandamano hayo ya wananchi, siku ya Jumatatu alikuwa chini ya vitisho na mashinikizo makali yanayomtaka ajiuzulu wadhifa wake. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania wamewahi mara kadhaa kuonyesha radiamali yao dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni na kutaka kukomeshwa kwa mauaji ya raia katika Ukanda wa Gaza. Kutokana na kufanyika maandamano ya amani katika chuo kikuu hiki, Liz Magill alikosolewa mno na waungaji mkono wa utawala ghasibu wa Israel.

Katika tukio jingine, wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Harvard waliitwa kwenye kamati ya nidhamu ya chuo kikuu kutokana na kuwaunga mkono watu wa Gaza na kushiriki katika mkusanyiko wa kulalamia mauaji ya Israel huko Gaza. Chuo Kikuu cha Harvard kimeeleza katika taarifa yake kwamba, kuandaliwa kwa maandamano ya wafuasi wa Palestina katika chuo kikuu hiki kuwa ni tabia isiyokubalika ambayo inazuia na kukwamisha shughuli za kawaida chuoni hapo. Inatarajiwa kuwa, wanachuo walioshiriki katika maandamano ya kuunga mkono Wapalestina katika Chuo Kikuu cha Harvard mwezi uliopita watapewa onyo.

Kojo Achampong mmoja wa wanachuo wa Chuo Kikuu cha Harvard anasema: Hatua za kinidhamu ambazo zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wanachi hao zinaweza kujumuisha kusimamishwa masomo. Hata hivyo, wanachofanya wao (wakuu wa vyuo vikuu) hakiwezi kutuzuia sisi na kwa hakika vitendo kama hivi haviwezi kutusimamisha na kutufanya tushindwe kusonga mbele katika njia ya kutangaza mshikamano na wananchi wa Palestina.

Wapalestina zaidi ya 18,000 wameuawa tangu Israel ilipoanza kufanya mashambulio ya kinyama huko Gaza

 

Licha ya uungaji mkono mkubwa wa serikali ya Demokrats ya Biden, ambayo inadai haki za binadamu kwa Israel, lakini ndani ya Marekani kwenyewe, watu na wasomi, hasa wanafunzi na maprofesa, wanapinga vitendo vya jinai vya Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kukomesha umwagaji damu ambao unaongezeka siku baada ya siku.

Kuhusiana na hilo, vyuo vikuu vya Marekani vimegeuka na kuwa uwanja wa makabiliano kati ya wafuasi wa taifa la Palestina na utawala wa Kizayuni, na katika wiki chache baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba na mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza, vimekuwa kitovu cha mikusanyiko dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Misimamo ya wahadhiri na maprofesa wa vyuo vikuu ya kuunga mkono Wapalestina na maandamano ya wanafunzi dhidi ya jinai za Israel imeongeza mashinikizo dhidi yao. Mashinikizo dhidi ya wasomi wa Marekani yanayoambatana na shutuma za chuki dhidi ya Wayahudi zimesababisha wengi wengi wao kuchukua njia ya kujidhibiti na hata kuepuka kutoa maoni ya kielimu kuhusu mizozo iliyotokea. Asilimia 80 ya maprofesa na wanafunzi wa masomo ya utambuzi wa Mashariki ya Kati nchini Marekani wanasema wanajizuia kutoa maoni kuhusu uhalifu na jinai za Israel.

Kupanuka wigo wa uungaji mkono kwa Wapalestina na kulaani vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Gaza hususan katika ngazi ya vyuo vikuu vya Marekani kwa upande mmoja, na hatua za duru na asasi zinazoiunga mkono Israel hususan katika Bunge la Marekani na asasi usimamizi wa vituo vya vyuo vikuu, kuwatisha wanafunzi na maprofesa na kuwatishia kuwafukuza na hata kutekelezwa hilo kwa rais wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania kwa upande wa pili, kwa mara nyingine tena kumetilia shaka madai ya uhuru wa kujieleza katika nchi za Magharibi na hasa nchini Marekani ambao umekuwa ukipigiwa upatu.