Hizbullah ya Lebanon yalenga maeneo ya Wazayuni
Hizbullah ya Lebanon imelenga maeneo kadhaa ya Wazayuni karibu na mpaka wa Lebanon na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Al-Mayadeen, Hizbullah ya Lebanon ilitangaza katika taarifa yake ya Jumatano kwamba imelenga kwa makombora ya Burkan mkusanyiko wa wanajeshi wa Kizayuni katika kambi ya Zabdin katika mashamba yaliyotekwa ya Shabaa na vituo vya kijeshi vya Israel huko Bayadh Belida na Al-Malkiyeh.
Kwa mujibu wa taarifa za Hizbullah ya Lebanon, vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni karibu na Roisat Al Alam katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu pia vimelengwa.
Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa, imerusha makombora katika mkusanyiko wa askari jeshi wa Kizayuni karibu na kambi ya Dovivo na kusisitiza kuwa, mashambulizi hayo yote yamesababisha uharibifu mkubwa kwa askari wa adaui na zana za kijeshi za utawala huo ghasibu wa Kizayuni.
Jeshi la Israel pia limeshambulia kwa mabomu eneo la karibu na mji wa Eita al-Sha'ab kwa mara 3 na mara 4 eneo la Al-Labuna, karibu na mpaka wa kusini wa Lebanon.
Makombora ya utawala wa Kizayuni pia yameshambulia maeneo ya Al-Naqourah na Al-Labuna kusini mwa Lebanon.
Kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya makundi ya muqawama ya Palestina, Hizbullah ya Lebanon iliuamua kuwashughulisha wanajeshi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa kuanzisha mashambulizi makali ya kila siku dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni ndani ya ardhi ya Palestina ili kupunguza mashinikizo dhidi ya wanamuqawama wa Ukanda wa Gaza.