OCHA: Israel inazuia kupelekwa dawa kaskazini mwa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107292-ocha_israel_inazuia_kupelekwa_dawa_kaskazini_mwa_gaza
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuzuia ufikishaji wa misaada muhimu ya kibinaadamu ikiwa ni pamoja na dawa muhimu na mafuta ya kuendesha huduma za maji na usafi wa mazingira kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-01-16T23:06:51+00:00 )
Jan 16, 2024 23:06 UTC
  • OCHA: Israel inazuia kupelekwa dawa kaskazini mwa Gaza

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuzuia ufikishaji wa misaada muhimu ya kibinaadamu ikiwa ni pamoja na dawa muhimu na mafuta ya kuendesha huduma za maji na usafi wa mazingira kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba, ukosefu wa vifaa hivi muhimu unaleta hatari kubwa za kiafya kwa watu waliozingirwa wa Ukanda wa Gaza.

Aidha kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), asilimia 40 ya wakazi milioni 2.3 wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya njaa. 

Kamishna Mkuu wa UNRWA amesema: Watu wa Palestina wanakabiliwa na machungu ya pamoja, na hakuna eneo salama katika Ukanda wa Gaza.

Jinai za Israel Gaza

Kabla ya hapo,  Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu (OCHR) ilisisitiza haja ya kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza, ili kuzuia kuendelea mauaji na mateso ya wananchi wakati vita vya utawala wa Israel dhidi ya eneo hilo vikiendelea kwa zaidi ya miezi mitatu.

Mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel mbali na kutoa roho za makumi ya maelfu ya Wapalestina, lakini pia yamesababisha sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza kuwa magofu.

Ripoti zinaeleza kuwa, asilimia 70 ya nyumba na majengo katika Ukanda wa Gaza zimebomolewa kufuatia mashambulizi hayo ya pande zote ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo.