Sababu za vita vya Gaza kuendelea kwa muda mrefu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107300-sababu_za_vita_vya_gaza_kuendelea_kwa_muda_mrefu
Licha ya kupita siku 100 tangu vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza vianze, lakini bado hakuna matarajio ya kumalizika kwa vita hivyo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jan 17, 2024 01:03 UTC
  • Sababu za vita vya Gaza kuendelea kwa muda mrefu

Licha ya kupita siku 100 tangu vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza vianze, lakini bado hakuna matarajio ya kumalizika kwa vita hivyo.

Katika kitabu chake kiitwacho "Crisis in World Politics", mwanafikra wa Canada Michael Brecher anafafanua mgogoro kuwa ni hali ambayo kupitia kwayo maadili na maslahi muhimu ya nchi yanatishiwa na serikali zinakabiliwa na mshangao wakati mgogoro unapotokea.

Michael Brecher anazingatia viashirio sita ili kubainisha ukubwa na ukali wa mgogoro, ambao ni umuhimu wa kijiografia, mada ya mgogoro, utumiaji mabavu kwa wachezaji na wahusika, idadi ya wachezaji, kutokuweko mlingano na kiwango cha kuingilia kati madola makubwa.

Kutumia nadharia ya Michael Brecher kuhusiana na vita vya Gaza inaonyesha ni kwa nini, kinyume na wazo la awali, vita hivi vinaendelea na hakuna matarajio ya mwisho wake.

Sababu ya kwanza ni umuhimu wa kijiografia na kistratejia wa Gaza. Gaza ni ukanda mdogo, lakini uko karibu na Palestina inayokaliwa kwa mabavu na inachukuliwa kuwa moja ya vituo kuu vya muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kwa muktadha huo kushindwa kwa utawala wa Kizayuni huko Gaza ni jambo lisilokubalika kwa utawala huu.

Sababu ya pili ni maudhui ya mgogoro. Ukweli ni kwamba suala kuu la vita vya Gaza ni kupoteza itibari ya utawala wa Kizayuni. Utawala huo ulikuwa na itibari ya hali ya juu ya kijeshi na kijasusi na kiujuma itibari ya kumzuia mtu kuishambulia. Lakini pigo la Kimbunga cha Al-Aqswa lilisambaratisha yote haya. Wakati huo huo, utawala huo umeshindwa kuwakomboa mateka wake wanaoshikiliwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika kipindi cha siku 100 zilizopita, jambo ambalo limetilia shaka zaidi itibari ya uwezo wa taarifa za kijasusi za Tel Aviv.

 

Sababu ya tatu ni utumiaji mabavu baina ya wachezaji na wahusika. Zaidi ya Wazayuni 1,500 waliuawa katika operesheni ya kimbunga ya Al-Aqsa. Suala hili pia halikubaliki kwa utawala wa Kizayuni ambao unakabiliwa na tatizo la idadi ya watu na umeufanya uungaji mkono wa wananchi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa moja ya nguzo za mafundisho yake ya kijeshi. Wakati huo huo, kiasi cha ukatili uliotumiwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza ni katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, jambo ambalo kivitendo liliifanya isiogope kuendelea kwa ghasia na mauaji ya kimbari.

Sababu ya nne ni wingi wa wachezaji. Ijapokuwa wahusika wakuu wawili wa vita hivyo ni utawala wa Kizayuni na harakati ya Hamas, lakini hawahesabiwi kuwa ndio wachezaji na wahusika wote wa vita hivi. Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zimeungana rasmi na utawala wa Kizayuni, Yemen na Hizbullah ya Lebanon pia zinaunga mkono Gaza na Hamas katika vita hivi.

Wakati idadi ya wahusika katika mgogoro inapokuwa kubwa, uwezekano wa kufikia makubaliano ya kumaliza mgogoro ni mdogo. Hata hivyo, idadi ya wahusika sio sababu kuu ya kurefushwa kwa vita vya Ghaza, bali kushindwa kwa utawala wa Kizayuni na Marekani kufikia malengo yao ya kijeshi ndio sababu muhimu ya kurefuka vita hivyo.

Wanamapambano wa HAMAS

 

Sababu ya tano ni kutokuweko mlingano. Uwezo wa kijeshi wa utawala haramu wa Israel na Harakatii ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS sio tu kwamba, haulingani bali hata haukaribiani. Utawala wa Kizayuni wa Israel unapatiwa himaya ya kisilaha ya pande zote ya Marekani na madola kadhaa ya Ulaya na kwa upande wa zana ni kwamba, suhula zake haziwezi kulinganishwa na zana za Hamas. Kutokuweko mlingano wa nguvu za kijeshi baina ya pande mbili ni sababu nyingine muhimu ya kuchukua muda mrefu vita hivyo.

Sababu ya sita ni kiwango cha uingiliaji kati wa madola makubwa. Uingiliaji wa madola makubwa katika vita vya Gaza haufanyiki tu katika fremu ya himaya ya vyombo vya habari na ya kisiasa, bali Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimegeuka na kuwa upande wa pili wa vita dhidi ya Gaza na zimekuwa zikitetea jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu huko Gaza. Utendaji huu wa kinafiki wa madola ya Magharibi ni sababu muhimu na ya kimsingi ya kuchukua muda mrefu vita vya Gaza na inaonekana kuwa, madhali mataifa hayo makubwa hayajaonyesha nia na azma thabiti ya kuhitimisha vita vya Gaza, vita hivyo haviwezi kufikia tamati katika siku za hivi karibuni.