Hizbullah yajibu mapigo, yapiga ngome za Israel kwa droni na mizinga
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imejibu jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa kupiga ngome na kambi za kijeshi za Wazayuni kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, kwa makombora ya mizinga na ndege zisizo na rubani (droni).
Kanali ya televisheni ya al-Mayadeen imenukuu taarifa ya Hizbullah inayosema kuwa, wanajihadi wa harakati hiyo ya muqawama jana Ijumaa walishambulia ngome ya Israel ya Ruwaisat al-Alam katika Milima ya Kfarshouba na kulisababishia hasara kubwa jeshi la utawala huo pandikizi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Hizbullah imeshambulia pia mkusanyiko wa wanajeshi wa Israel waliokuwa katika kambi ya kijeshi ya Jal al-Alam karibu na kijiji cha Alma al-Shaab, kusini mwa Lebanon.
Kadhalika wanamapambano wa Hizbullah wameshambulia na kukiteketeza kifaru cha kijeshi cha Israel katika kituo cha kijeshi cha Metula kwa kutumia ndege isiyo na rubani (droni).
Hivi karibuni, vyombo vya habari vya Kizayuni vilitangaza kuwa, wanajeshi 17 wa utawala wa haramu wa Israel wameangamizwa katika mashambulizi ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon tokea Oktoba 7, 2023 hadi sasa. Hizbullah ya Lebanon imesisitiza kuwa, harakati hiyo ya muqawama inafanya mashambulizi yake dhidi ya Wazayuni kujibu mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kwamba uungaji mkono wa kivitendo wa Hizbullah kwa wakazi wa Gaza utaendelea.
Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon imewasilisha faili la malalamiko dhidi ya Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa hatua ya utawala wa Kizayuni kukiuka anga ya nchi hiyo ya Kiarabu. Hii ni baada ya ndege za kivita za Israel kushambulia mji wa Aita al-Shaab, kusini mwa Lebanon.
Aidha vifaru na mizinga ya Wazayuni imeshambulia nyumba na makazi ya raia katika mji wa al-Khiam town, karibu na Milima ya Hamames, viungani mwa mji wa al-Odaisseh na vijiji vya Kfarkela.