Wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa Bahrain waivunjia heshima Qur'ani Tukufu
Wanajeshi wa utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain, wamekivunjia heshima Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwa kukichanachana.
Mtandao wa habari wa 'Bahrain al-Yaum' umeripoti kuwa, askari kadhaa wa usalama wa utawala huo unaopata himaya kamili kutoka kwa Saudia na nchi za Magharibi, walivamia seli maalumu za gereza wanamozuiliwa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo katika jela ya Jau (Jaw) na kuanza kuchanachana vitabu vya Qur'ani Tukufu pamoja na vitabu vingine vya kidini vilivyokuwepo eneo hilo bila ya sababu yoyote.
Kufuatia tukio hilo chungu, wafungwa wa jela hiyo sambamba na kulaani kitendo hicho, wamefanya mgomo wa kulalamikia kuvunjiwa heshima kitabu cha Qur'ani Tukufu. Kabla ya hapo utawala huo wa Aal-Khalifa, uliibua hasira za Waislamu ndani na nje ya nchi hiyo kufuatia hatua ya askari wake ya kubomoa misikiti kadhaa na Husseiniyyah, sambamba na kuchoma moto nakala kadhaa za Qur'ani ambacho ni kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu.
Maulama wa Bahrain sambamba na kulaani vitendo hivyo vya kubomoa nyumba za ibada na kuchoma moto Qur'an Tukufu, waliitaka jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa kuzuia kuvunjiwa matukufu hayo ya Waislamu.