Al-Shehabi: Uingereza inataka kuimarisha uhusiano wake na madikteta wa eneo
Katibu Mkuu wa Harakati ya Uhuru ya Bahrain amesema Uingereza inataka kuendeleza sera zake za kushupalia vita katika eneo la Mashariki ya Kati kwa ajili ya kujiongezea pato.
Dakta Saeed al-Shehabi ameyasema hayo kufuatia safari ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May nchini Bahrain kwa madhumuni ya kushiriki kikao cha 37 cha wakuu wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi P (GCC) na kusisitiza kuwa sera hizo hazitakuwa na tija na athari chanya kwa mustakabali wa uchumi wa Uingereza kwa sababu mbinu hiyo ya kupatia chumo haidumu kwa muda mrefu.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Uhuru ya Bahrain ameashiria matamshi ya Waziri Mkuu wa Uingereza kuhusu kudhamini amani na usalama wa Bahrain na kueleza kwamba nia ya Uingereza si kuhakikisha amani na usalama wa wananchi wa Bahrain bali ni kudhamini usalama wa utawala wa Aal Khalifa.
Al-Shehabi ameongeza kuwa kama wanajeshi wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Uingereza hawatoulinda na kuuhami utawala wa Aal-Khalifa utawala huo hautoweza kudumu nchini Bahrain.
Uingereza imeziuzia nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudia na Bahrain silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola zinazotumika kuwakandamiza raia wa nchi hizo.
Ikumbukwe kuwa Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.../