Nasrullah: Misimamo ya kuchupa mipaka inataka kuchafua taswira halisi ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21991-nasrullah_misimamo_ya_kuchupa_mipaka_inataka_kuchafua_taswira_halisi_ya_uislamu
Katibu Mkuu wa Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah amesema harakati za magenge ya kigaidi na kitakfiri yanayofanya jinai za kutisha eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika hazina mafungamano yoyote na Uislamu na shakhsia wake mbora na mtukufu, Bwana Mtume Muhammad SAW.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2016 12:54 UTC
  • Nasrullah: Misimamo ya kuchupa mipaka inataka kuchafua taswira halisi ya Uislamu

Katibu Mkuu wa Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah amesema harakati za magenge ya kigaidi na kitakfiri yanayofanya jinai za kutisha eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika hazina mafungamano yoyote na Uislamu na shakhsia wake mbora na mtukufu, Bwana Mtume Muhammad SAW.

Akihutubia kupitia mawasiliano ya video katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Sayyid Hassan Nasrullah amesema jitihada za kuuchafua Uislamu zimeingia katika marhala nyingine, ambapo Waislamu wote wanatwikwa lawama na kubebeshwa dhima ya jinai zinazofanywa na megenge ya wakufurishaji katika sehemu mbali mbali duniani.

Katibu Mkuu wa harakati ya mapambano ya Hizbullah amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapasa ifahamu kuwa, jinai zinazofanywa na magaidi na wenye misimamo ya kufurutu ada hazina uhusiano wowote na Uislamu na mafundisho ya dini hiyo tukufu.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah

Kadhalika Sayyid Nasrullah ambaye maudhui yake ya "Elimu na Jihadi" imelenga zaidi wanachuo amebainisha kuwa, harakati ya Hizbullah inaheshimu na kuona fahari kwa wanamapambano wenye kuendeleza harakati za kimuqawama katika sehemu yoyote ile duniani. 

Amesema ni jambo la kusikitisha namna Mawahabi na idiolojia yao ya utakfiri wamefumbia macho changamoto halisi zinazokabili Ulimwengu wa Kiislamu kama kadhia ya Palestina.

Sayyid Hassan Nasrullah amesema: "Dini yetu na Mtume wetu SAW vimechafuliwa na kupakwa matope katika miaka ya hivi karibuni. Jinai zinazofanywa na makundi ya kitakfiri na kiwahabi ndiyo maafa makuu dhidi ya misingi ya ubinadamu na utamaduni."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, juhudi zozote za kujaribu kuoanisha kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh au kundi jingine lolote la kigaidi na Uislamu ni hujuma dhidi ya dini hiyo tukufu na kwamba hakuna dini yoyote ya mbinguni inayoweza kuunga mkono jinai za magenge hayo ya kigaidi yenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Utakfiri kwa jina la Uislamu