Lavrov aitaka Uturuki kukoma kutuma silaha kwa makundi ya kigaidi Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2278-lavrov_aitaka_uturuki_kukoma_kutuma_silaha_kwa_makundi_ya_kigaidi_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametaka kuchukuliwe hatua za kuzuia magendo ya silaha kutoka Uturuki kwenda Syria ambako zinatumiwa na makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2016 03:21 UTC
  • Lavrov aitaka Uturuki kukoma kutuma silaha kwa makundi ya kigaidi Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametaka kuchukuliwe hatua za kuzuia magendo ya silaha kutoka Uturuki kwenda Syria ambako zinatumiwa na makundi ya kigaidi.

Sergei Lavrov amekiambia kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba, Uturuki inayaunga mkono na kuyasaidia moja kwa moja makundi ya kigaidi huko Syria na kwamba hatua za Uturuki zinahatarisha mpango wa amani wa Syria ulioanza kutekelezwa siku chache zilizopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema, kwa sasa lengo kuu ni kuzuia kutumwa silaha kwa makundi ya kigaidi huko Syria na kwamba ili kufanikisha lengo hilo kuna ulazima wa kufungwa mpaka wa Uturuki na Syria ambao unatumiwa kwa ajili ya kutuma silaha kwa magaidi. Ameongeza kuwa, Uturuki inatuma silaha hizo kwa makundi ya kigaidi chini ya mwavuli wa misaada ya kibinadamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Uturuki inawafuatilia na kuwafunga jela waandishi habari wanaofichua operesheni zake za kutuma silaha kwa makundi ya kigaidi ya Syria na kwamba hiyo ndiyo hali ya uhuru wa kusema na kujieleza nchini Uturuki.