Uingereza yakiri kuiuzia Saudi Arabia mabomu ya vishada 500
Uingereza imekiri kwamba, iliiuzia Saudi Arabia mamia ya mabomu ya vishada katika miaka ya 80, ambayo yumkini yanatumika katika hujuma za Riyadh nchini Yemen.
Barua ya Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Michael Fallon kwa mbunge wa chama cha kihafidhina nchini humo, Philip Hollobone imefichua kuwa, London iliiuzia Riyadh mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada aina BL755 kati ya mwaka 1986 na 1989.
Mwezi uliopita, waziri huyo alikiri kuwa silaha hizo haramu walizouuzia utawala wa Aal-Saud zimekuwa zikitumika 'kwa kiwango cha chini' nchini Yemen.
Tobias Ellwood, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza jana Jumanne aliliambia Bunge la nchi hiyo kuwa, ingawaje Saudia iliahidi kutotumia tena silaha hizo haramu dhidi ya wananchi wa Yemen, lakini haijathibitisha kuwa imeziharibu silaha zenyewe.
Mwezi uliopita wa Disemba, Ahmed al-Asiri, msemaji wa vikosi vya jeshi la Saudia nchini Yemen alisema ni kweli muungano wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh dhidi ya Yemen umetumia mabomu ya vishada yaliyotengenezwa Uingereza aina ya BL755.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yamekuwa yakizitaka Uingereza na Marekani zisimamishe uzalishaji na uuzaji wa mabomu ya vishada kinyume na sheria za kimataifa kwa Saudia, na yanautaka utawala wa Aal-Saud kukoma kutumia mabomu hayo haramu dhidi ya raia wasio na hatia nchini Yemen.
Watu zaidi ya 11,400 wameuwa katika hujuma za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia nchini Yemen, mbali na kuharibiwa asilimia kubwa ya miundomsingi, tangu Machi mwaka 2015.