Nasrullah: Israel itajuta kwa kutaka kulisukuma eneo katika vita
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ametahadharisha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya 'jahili' Benjamin Netanyahu unataka kulisukuma eneo la Mashariki ya Kati katika vita.
Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo leo Jumapili kwa mnasaba wa Siku ya Ashura inayoadhimishwa kote duniani na kufafanua kuwa, Netanyahu anapanga njama za kuhakikisha kuwa vita vipya vinashuhudiwa katika eneo hili.
Amesema: "Utawala wa Kizayuni hauna picha ya taathira hasi za mpango wake wa kutaka kulisukuma eneo katika vita. Hawajui nini kinachowasubiri iwapo watasonga mbele na azma yao hiyo ya kuchochea mapigano."
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, iwapo vita vipya vitatokea katika eneo, basi walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu wajiandae kwa maafa na mabalaa makubwa yanayowasubiri.
Ameonya kuwa, wakati vita vipya dhidi ya Lebanon na nchi nyingine za eneo vinavyochochewa na Israel vitakapoanza, basi Wazayuni hawatakuwa na wakati wala pahala pa kukimbilia.
Kwengineko katika hotuba yake, Sayyid Hassan Nasrullah amelitaja kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) kama tishio kuu katika eneo; na zimwi ambalo limechafua taswira ya dini tukufu ya Uislamu.
Kadhalika amewapongeza wananchi wanamuqawama wa Yemen kwa kusimama kidete na kutotetereshwa na uvamizi wa muungano wa kijeshi wa Aal-Saud dhidi yao, tangu Machi mwaka 2015; huku akisisitiza kuwa, idiolojia ya Kiwahabi inayoenezwa na watawala wa Riyadh ndio chanzo cha migogoro katika eneo hili.