Lebanon yakamata genge la majasusi wa Mossad
Vikosi vya usalama vya Lebanon vimetangaza kukamata genge lenye mfungamano na shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel, Mossad.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Akhbar toleo la Jumamosi, vikosi vya usalama vya Lebanon hivi karibuni vimefanikiwa kuwakamata wanachama wa genge linalofungamana na Mossad katika eneo la Burj El Barajneh kusini mwa Beirut. Taarifa zinasema genge hilo lilikuwa linakusanya taarifa za siri zinazohusiana na Harakati ya Hizbullah na kuzikabidhi kwa shirika la kijasusu la Mossad.
Katika oparesheni maalumu ya Ijumaa usiku, vikosi vya usalama vya Lebanon awali viliwakamata washukiwa wawili hapo Burj El Barajneh kusini mwa Beirut na mtu mwingine mmoja katika kijiji cha Deir Qubool.

Katika miezi ya hivi karibuni vikosi vya usalama vya Lebanon vimefanikiwa kuwakamata watu wengi ambao walikuwa wanashirikiana na shirika la kijasusu la Mossad ambao aghalabu walikuwa wanakusanya taarifa za siri kuhusu Harakati ya Hizbullah.
Hivi karibuni Yossi Cohen, mkuu wa shirika la Mossad alikiri kuwa shirika hilo linatekeleza maelfu ya oparesheni za kigaidi katika nchi mbali mbali duniani.