Israel: Tunapanga kumuua Nasrullah katika vita vijavyo dhidi ya Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36911-israel_tunapanga_kumuua_nasrullah_katika_vita_vijavyo_dhidi_ya_lebanon
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limetishia kwamba Sayyid Hasssan Nasrullah, kiongozi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon yupo kwenye shabaha ya kuuawa katika vita vijavyo vya Tel Aviv dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2017 04:16 UTC
  • Israel: Tunapanga kumuua Nasrullah katika vita vijavyo dhidi ya Lebanon

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limetishia kwamba Sayyid Hasssan Nasrullah, kiongozi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon yupo kwenye shabaha ya kuuawa katika vita vijavyo vya Tel Aviv dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Hayo yamesemwa na Brigedia Jenerali, Ronen Manelis, msemaji wa jeshi la Israel ambaye ameongeza kuwa, kuuawa Sayyid Nasrullah kutaathiri kampeni ya tawi la kijeshi la harakati hiyo.

Amesema Israel haina taswira ya nani ataibuka mshindi katika vita vijavyo dhidi ya Lebanon, lakini ina uhakika kuwa Nasrullah ndio shabaha na mlengwa mkuu wa vita hivyo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Jenerali Joseph Aoun, Mkuu wa Jeshi la Lebanon kuwataka wanajeshi wa nchi hiyo kuwa katika hali ya tahadhari hususan katika maeneo ya mpaka wa kusini, ili kuzima chokochoko zozote zinazoweza kuanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Israel inajiandaa kuishambulia Lebanon

Aidha kabla ya hapo, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Hizbullah Sheikh Nabil Qauoq alisema kuwa, harakati hiyo iko tayari kwa ajili ya makabiliano yoyote ya kijeshi, huku kukiwa na taarifa kuwa Saudi Arabia inauchochea utawala wa Kizayuni wa Israel uishambulie Lebanon kijeshi. 

Itakumbukwa kuwa, utawala haramu wa Israel umekuwa ukianzia uvamizi na vita vya mara kwa mara vikiwemo vile vya mwaka 2000 na 2006 dhidi ya Lebanon. Hata hivyo imekuwa ikipata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa Kiislamu wa Hizbullah. Kipigo kikali ilichokipata Israel katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006 kutoka kwa Hizbullah ya Lebanon kumeutia woga mkubwa utawala dhalimu wa Kizayuni na kuufanya uogope sana kuanzisha vita vipya.