Afisa wa MOSSAD akiri nguvu za Hizbullah ya Lebanon
-
Makomandoo wa utawala wa Kizayuni wakivamia Lebanon 1997 kabla ya kupata kipigo kikali kutoka kwa Hizbullah
Afisa mmoja wa shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD amekiri kwamba kushindwa operesheni ya utawala huo ya mwaka 1997 kulitokana na Hizbullah kuwa na teknolojia kubwa zaidi iliyoiwezesha kupenya kusikiliza mazungumzo ya maafisa wa Israel.
Amiram Levin, mkuu wa zamani wa MOSSAD na kamanda wa zamani wa eneo la kaskazini la utawala wa Kizayuni amefichua kuwa, katika operesheni ya Ansariya ya mwaka 1997, Hizbullah ya Lebanon ilifanikiwa kupenya na kusikiliza mazungumzo ya marubani wawili wa Israel na ikawawekea mtego makomandoo wa Israel kabla ya kufika sehemu ya operesheni hiyo.
Televisheni ya al Alam imeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, ufichuaji huo wa mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Israel MOSSAD umetolewa katika filamu ya matukio ya kweli iliyorushwa hewani na televisheni ya al Mayadeeni chini ya kicha cha maneno: Kinamasi cha Israel Kusini.
Operesheni ya Ansariya ni moja ya operesheni maarufu zaidi zilizofanywa na Hizbullah katika kipindi chote hiki cha miaka 20 iliyopita huko kusini mwa Lebanon. Wanamapambano wa Hizbullah waliweka mtego katika njia iliyotumiwa na kundi la makomandoo 15 wa kikosi maalumu cha jeshi la Israel katika kijiji cha Ansariya, kusini mwa Lebanon na kutoa pigo kali kwa Wazayuni hao wavamizi.

Baada ya kupita muda, Hizbullah ya Lebanon ilibadilishana na Israel miili iliyoangamizwa ya makomandoo hao wa Kizayuni katika mkabala wa kupewa miili 40 ya mashahidi wa Lebanon ambapo 30 kati yao walikuwa ni mashahidi wa muqawama wa Kiislamu.