Onyo la Hizbullah ya Lebanon kwa Marekani, Israel na Saudi Arabia
Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon amesisitiza kuwa, Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia haziwezi kukaa kimya baada ya kushindwa njama zao katika nchi za Iraq, Syria na Lebanon.
Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo Jumanne katika kongamano kubwa la uchaguzi mkoani Beqaa huko Lebanon na kusema kuwa, kuna baadhi ya vyama na mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo inaunga mkono magaidi.
Uchaguzi wa Bunge unatarajiwa kufanyika tarehe 6 mwezi huu wa Mei huko nchini Lebanon. Matukio ya nchi hiyo yanaonesha kwamba, uchaguzi huo utaathiriwa sana na matukio ya eneo la Mashariki ya Kati kama ambavyo nao utayaathiri matukio ya eneo hili nyeti, na hilo linaonesha namna Lebanon ilivyo na umuhimu mkubwa. Umuhimu wa Lebanon kabla ya jambo lolote unatokana na kuwemo Hizbullah katika muundo wa kiutawala, kiulinzi na kisiasa ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu na nafasi yake katika mlingano wa nguvu kwenye zima la Mashariki ya Kati. Hizbullah imekuwa na mchango mkubwa katika kuwashinda nguvu magaidi huko Syria na Lebanon sambamba na kufelisha njama za madola ya kibeberu yanayopenda kujipanua katika nchi hizo mbili za Kiarabu.
Mafanikio hayo yamevutia hisia za wapiga kura wengi wa Lebanon. Muqawama na kusimama kitede wananchi wa Lebanon wakiongozwa na Hizbullah hakukufanikiwa tu katika vita dhidi ya ugaidi, lakini pia kumeonesha mafanikio makubwa katika kupambana na ubeberu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufanikiwa kuufurusha utawala huo vamizi katika ardhi ya Lebanon. Mafanikio hayo makubwa ya Hizbullah yamewakasirisha sana maadui ambao kila kukicha wanaongeza njama zao dhidi ya harakati hiyo ya Kiislamu vikiwemo vita vya kipropaganda na kutoa tuhuma zisizo na msingi. Hata hivyo njama zote hizo zimeshindwa kutokana na hekima na siasa sahihi za Hizbullah za kuwashirikisha vilivyo wananchi katika mambo yake na kupelekea kupendwa na wananchi hao wa Lebanon ambao wanaamini kuwa harakati hiyo ni yao wao wenyewe na si ya kupandikizwa kutoka nje. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni ukaonesha kuwa nafasi ya Hizbullah itaimarika zaidi katika uchaguzi ujao wa Bunge la Lebanon.
Msimamo mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ni kuleta mshikamano wa kisiasa nchini humo kwa kuwashirikisha kikamilifu wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa na kidini. Msimamo huo umesimama juu ya msingi wa kushikamanisha barabara vitu vitatu ambavyo ni muqawama, jeshi na wananchi kwani ni mshikamano huo ndio ulioweza kuilinda vizuri Lebanon mbele ya njama za maadui. Mafanikio ya mshikamano huo yako wazi kwa kila mtu huko Lebanon. Ni mafanikio hayo ndiyo yaliyowafanya wapiga kura nchini humo wawapime wanasiasa kwa mtazamo huo kwani wanaamini kuwa ndio unaoweza kuwadhaminia usalama wao mbele ya njama za kila namna za Marekani, Israel na vibaraka wao. Kiujumla ni kwamba ushindi uliopatikana katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi huko Iraq, Syria na Lebanon si tu umeonesha kufeli siasa za kundi la mhimili wa shari unaoundwa na Marekani, Israel na Saudi Arabia za kutumia magenge ya kigaidi kufanikishia malengo yao haramu, lakini pia ushindi huo umeuandalia mazingira mazuri muqawama, wa kupata mafanikio makubwa katika uga wa kisiasa.
Kiujumla ni kwamba eneo la Mashariki ya Kati ni muhimu sana duniani na ndio maana njama za kila namna zinaelekezwa kwenye eneo hili nyeti. Njama mpya kabisa ni kile kilichozushwa hivi sasa na Marekani, Israel na Saudi Arabia kinachodaiwa eti ni "Mapatano ya Karne" ambayo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa lengo la njama hizo mpya ni kuiangamiza kikamilifu Palestina na kufuta kabisa neno taifa la Palestina katika uso wa dunia. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akayalaani vikali 'Mapatano ya Karne' na kusisitiza kuwa, kamwe mamlaka hiyo haitakubali kuwa na nchi ya Palestina yenye mipaka ya muda.
Kwa kumalizia tunaweza kusema kuwa, mrengo wa muqawama unaopigwa vita mno na Saudi Arabia, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel umethibitisha nguvu na uwezo wake si katika medani za mapambano ya kijeshi tu, bali pia katika nyuga nyinginezo za kielimu, kiuchumi na kisiasa kama ambavyo pia mrengo huo ni kizuizi kikuu cha kufelisha njama za mabeberu na vibaraka wao katika eneo hili. Na ni sawa kabisa alivyotahadharisha Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, kwamba mhimili wa shari yaani Marekani, Israel na Saudi Arabia haziwezi kukaa kimya baada ya kuona njama zao zote zimefeli katika eneo hili.