UAE ilitumia spyware ya Israel kuwafanyia ujasusi viongozi wa eneo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47831-uae_ilitumia_spyware_ya_israel_kuwafanyia_ujasusi_viongozi_wa_eneo
Utawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulitumia programu ya kijasusi ya kudukua kompyuta au simu za mkononi (spyware) kuwafanyia ujasusi viongozi kadhaa wa nchi za Kiarabu akiwemo Amir wa Qatar, Waziri Mkuu wa Lebanon na mwanamfalme mmoja wa Saudia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2018 09:33 UTC
  • UAE ilitumia spyware ya Israel kuwafanyia ujasusi viongozi wa eneo

Utawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu ulitumia programu ya kijasusi ya kudukua kompyuta au simu za mkononi (spyware) kuwafanyia ujasusi viongozi kadhaa wa nchi za Kiarabu akiwemo Amir wa Qatar, Waziri Mkuu wa Lebanon na mwanamfalme mmoja wa Saudia.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, shirika la programu za kompyuta la NSO Group ambalo liko katika utawala wa Kizayuni wa Isael lilishiriki katika hujuma ya intaneti dhidi ya watu ambao UAE inawatazama kama mahasimu. Hujuma hiyo ilitekelezwa kwa kutumia programu ya Pegasus ya ujasusi ambayo ilibadilisha simu erevu au smartphone ya mlengwa kuwa chombo cha ujasusi.

Tayari raia wa Qatar, waandishi habari wawili wa Mexico na watetezi wa haki za binadamu wameshawasilisha mashtaka dhidi ya shirika hilo huko Israeli na Cyprus.

Ushahidi unaonyesha kuwa UAE ilianza kutumia rasmi spyware ya Pegasus ya NSO Agosti 2013. Mwaka 2014 UAE ilitaka shirika hilo lifanye ujasusi katika simu za mkononi za Amir wa Qatari Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri, Mwanamfalme wa Saudia Mutaib II bin Abdullah bin Abdulaziz Al Saud, ambaye alikuwa mkuu wa gadi ya kitaifa na Abdulaziz al-Khamis, mhariri wa gazeti la Al-Arab ambalo liko mjini London.

Baada ya siku nne shirika hilo la Israel liliwatumia wakuu wa UAE baruapepe iliyokuwa na mafaili mawili ya sauti ya simu za Khamis na hivyo wakuu wa UAE wakaanza ushirikiano kamili na shirika hilo.

Pegasus huambukiza simu ya mwenye kulengwa kwa kumtumia ujumbe wenye kumshawishi kubonyeza na kufungua kiungo. Baada ya hapo mwenye kufanya ujasusi huweza kufuatilia kila kitu katika simu ya mkononi na hata mazungumzo ya eneo lililo karibu na simu.