Baada ya Imarati, Bahrain nayo yafungua tena ubalozi wake Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50477-baada_ya_imarati_bahrain_nayo_yafungua_tena_ubalozi_wake_syria
Serikali ya Bahrain imefuata nyayo za Umoja wa Falme za Kiarabu na kufungua tena ubalozi wake katika mji mkuu wa Syria, Damascus, baada ya kupita zaidi ya miaka saba tangu ulipoanza mgogoro wa ndani katika nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 28, 2018 12:29 UTC
  • Baada ya Imarati, Bahrain nayo yafungua tena ubalozi wake Syria

Serikali ya Bahrain imefuata nyayo za Umoja wa Falme za Kiarabu na kufungua tena ubalozi wake katika mji mkuu wa Syria, Damascus, baada ya kupita zaidi ya miaka saba tangu ulipoanza mgogoro wa ndani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Taarifa iliyorushwa na shirika rasmi la habari la Bahrain BNA imesema kuwa, "Utawala wa Kifalme wa Bahrain umetangaza kuwa shughuli za kawaida zinaendelea katika ubalozi wake katika taifa dugu la Jamhuri ya Kiarabu ya Syria."

Manama imesema lengo la kufungua tena ubalozi wake mjini Damascus ni kuhakikisha kuwa mataifa ya Kiarabu yanashirikiana na kufanya kazi bega kwa bega, ili kuzuia uingiliaji wa mambo ya ndani ya Syria, sambamba na kurejesha usalama na uthabiti katika nchi hiyo.

Hatua ya Manama kufungua upya ubalozi wake nchini Syria imechukuliwa siku moja baada ya Imarati kufungua tena ubalozi wake katika mji mkuu wa nchi hiyo Damascus.

Ubalozi wa UAE mjini Damascus

Imarati na Bahrain, kama nchi nyingine za Kiarabu zilifunga balozi zao mjini Damascus muda mfupi baada ya kuanza mgogoro wa Syria mwaka 2011. 

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa majeshi ya nchi hiyo yataondoka katika ardhi ya Syria.

Disemba 16, Rais Omar al-Bashir wa Sudan alifanya safari nchini Syria na kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuitembelea nchi hiyo; siku chache baada ya Bunge la Arab League kutaka Syria irejeshwe kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.