Hizbullah: Israel itaangamia ikithubutu kuishambulia Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53244-hizbullah_israel_itaangamia_ikithubutu_kuishambulia_lebanon
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ameutahadharisha utawala wa Tel Aviv dhidi ya kuanzisha vita vipya dhidi ya Lebanon na kusisitiza kuwa, wanajeshi wa utawala haramu wa Israel watasambaratishwa na kuangamizwa iwapo vita hivyo vitaibuka.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
May 03, 2019 03:15 UTC
  • Hizbullah: Israel itaangamia ikithubutu kuishambulia Lebanon

Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ameutahadharisha utawala wa Tel Aviv dhidi ya kuanzisha vita vipya dhidi ya Lebanon na kusisitiza kuwa, wanajeshi wa utawala haramu wa Israel watasambaratishwa na kuangamizwa iwapo vita hivyo vitaibuka.

Sayyid Hasssan Nasrullah aliyasema hayo jana Alkhamisi wakati akihutubu kupitia njia ya televisheni katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut na kubainisha kuwa, "Israel inafahamu fika kuwa, vita vyovyote dhidi ya Lebanon vinahitaji maamuzi na mahesabu ya kina. Hizbullah ipo tayari kwa ajili ya kujibu chochoko zozote. Utawala wa Kizayuni unaogopa kuanzisha vita vipya hata katika Ukanda wa Gaza, achilia mbali Lebanon."

Amesema bayana kuwa, "Vikosi vyote vya utawala haramu wa Israel vitaangamizwa mbele ya macho ya vyombo vikuu vya habari na dunia yote kwa ujumla iwapo vitathubutu kutia mguu katika ardhi ya Lebanon. Hatuwezi kusalimisha hata shibri moja ya ardhi ya Lebanon."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, "Utawala wa Kizayuni hauna picha ya taathira hasi za mpango wake wa kutaka kulisukuma eneo katika vita. Hawajui nini kinachowasubiri iwapo watasonga mbele na azma yao hiyo ya kuchochea mapigano."

Sehemu ya zana za kivita za Hizbullah ya Lebanon

Ameongeza kuwa, wanamuqawama wa Hizbullah waliingia Syria kwa ajili ya kuzima njama na chokochoko za Marekani, Israel na Saudi Arabia, na kwamba kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) halingeweza kuteka na kuthibiti kipande chochote cha ardhi za Syria na Iraq bila ridhaa, baraka na uungaji mkono wa pande tatu hizo za shari, likishajiishwa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Wamagharibi.

Itakumbukwa kuwa, utawala haramu wa Israel umekuwa ukianzisha uvamizi na vita vya mara kwa mara vikiwemo vile vya mwaka 2000 na 2006 dhidi ya Lebanon. Hata hivyo umekuwa ukipata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa Kiislamu wa Hizbullah.