Nasrallah: Hizbullah itajibu vikali uchokozi wowote wa utawala wa Israel
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na chokochoko zake dhidi ya Lebanon, na kusema: "Uchokozi wa Israel utapata jibu kali kutoka kwa harakati ya muqawama (Hizbullah)."
Sayyid Hassan Nasrallah aliyasema hayo Jumatatu usiku alipohutubu mubashara kupitia Televisheni ya Al Manar na kusema, zile zama ambazo utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa unakiuka mipaka ya Lebanon bila kujali sasa zimefika ukingoni. Ameongeza kuwa: "Uungaji mkono wa serikali, jeshi na watu wa Lebanon kwa oparesheni ya hivi karibuni ya Muqawama (Hizbullah) ni jambo ambalo limethibitisha kuwa, Hizbullah ina uungaji mkono imara katika kujibu vitisho vya Wazayuni."
Katibu Mkuu wa Hizbullah ameashiria oparesheni iliyofeli ya wiki iliyopita ya drone vamizi za utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la kusini mwa Beirut na kusema kutokana na kuwa macho Hizbullah pamoja na jeshi la Lebanon, ardhi ya Lebanon haitakuwa tena eneo la jeshi la Israel kuibua chokochoko zake.
Sayyid Hassan Nasrallah ameendelea kusema kuwa hivi sasa Hizbullah ina uwezo wa kutekeleza mashambulizi hadi katika mji wa Tel Aviv.
Ikumbukwe kuwa siku ya Jumapili, wapiganaji shupavu wa Hizbullah walitekeleza oparesheni ambayo ilipelekea kuangamizwa gari la deraya la jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika barabara ya kituo cha kijeshi cha Avivim. Katika taarifa, Hizbullah ilitangaza kuwa, katika oparesheni hiyo wanajeshi kadhaa wa Kizayuni waliuawa na kujeruhiwa.
Oparesheni hiyo ya Hizbullah ilikuwa ya kulipiza kisasi baada ya drone mbili vamizi za utawala wa Kizayuni wa Israel kukiuka anga ya Lebanon na kuanguka katika eneo la kusini mwa Beirut.