Wakurdi wa Syria wamedai kuwauwa wanajeshi 75 wa Uturuki
Wanamgambo wa Kikurdi kwa jina la Vikosi vya kidemokrasia vya Syria (QASD) leo vimedai kuwa, vimewaua wanajeshi 75 wa Uturuki na kuangamiza pia vifaru vyao 7 katika mapigano yaliyojiri katika mji wa Ra's al Ayn kaskazini mwa Syria.
Wanajeshi wengine 19 wa Uturuki wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo huko Ra's al Ayn. Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi ya Uturuki leo imetangaza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo na wanamgambo wanaoungwa mkono na nchi hiyo hivi sasa wanaudhibiti kikamilifu mji wa Ra's al Ayn huko al Hasakah hata hivyo taarifa hii imepingwa na duru za Wakurdi.
Katika upande mwingine, shirika la habari la Anatolia la Uturuki leo limetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limekikomboa kijiji cha Suluk katika mji wa Tel Abid mashariki mwa Mto Furati kutoka mikononi mwa makundi ya wanamgambo wa Kikurdi ya YPG na PKK.
Shirika la habari la Anatolia limeongeza kuwa, jeshi la Uturuki pamoja na jeshi la ukombozi wa Syria linaloungwa mkono na Uturuki yanazidi kusonga mbele na kukomboa maeneo mapya yaliyokuwa yakishikiliwa na magaidi.
Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imeadai kuwa wanamgambo wa Kikurdi zaidi ya 400 wameuliwa hadi sasa tangu kuanza mashambulizi ya nchi hiyo kaskazini mwa Syria.
Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki tarehe kumi mwezi huu Jumatano iliyopita aliamuru rasmi kuanza kutekelezwa mashambulizi katika maeneo ya kaskazini mwa Syria katika oparesheni iliyopewa jina la "Chemchemi ya Amani". Uturuki imesema kuwa mashambulizi hayo yanatekelezwa ili kuyalenga makundi ya YPG, PKK na Daesh.