Jan 05, 2020 16:18 UTC
  • Bunge la Iraq lapitisha mpango wa kuwatimua askari wa jeshi la Marekani walioko nchini humo + Video

Bunge la Iraq limepiga kura na kupitisha mpango uliopendekezwa na wabunge wa kuhitimisha makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na Marekani na kuwataka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo.

Katika kikao chao cha dharura kilichofanyika leo Jumapili, wabunge hao akthari wa wabunge wamepigia kura ya 'ndiyo' mpango huo unaotaka vikosi vya jeshi la Marekani viondoke nchini humo.

Akizungumza katika kikao cha upigaji kura wa kupitisha mpango huo wa kuvitaka vikosi vya majeshi ya kigeni yaondoke nchini humo, Waziri Mkuu wa serikali ya muda ya Iraq, Adil Abdul-Mahdi ametaka majeshi ya Marekani yaondoke haraka nchini Iraq na kusisitiza kwa kusema:" Ni kwa manufaa ya Iraq na Marekani vikosi vya kigeni kuondoka nchini Iraq."

Abdul-Mahdi amesema: Kuwepo kijeshi Marekani nchini Iraq ni kwa ajili ya kupambana na Daesh na kutoa mafunzo kwa vikosi vya Iraq; lakini akafafanua kwamba, mtazamo ilionao Marekani kwa Iraq kuhusiana na sera zake kuhusu Iran haukubaliki, na akaongeza kwamba: "Hatukubaliani na sera nyingi  za Marekani kuhusu Iraq."

Waziri Mkuu wa seriikali ya muda ya Iraq amebainisha kuwa: Marekani haikuomba radhi kwa kuvishambulia vituo vya harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi katika mji wa al-Qaim na akaongeza kwamba: "Iran imepambana na ugaidi na kuvisaidia vikosi vya usalama vya Iraq; na Al-Hashdu-Sha'abi ni sehemu ya mfumo wa usalama wa Iraq."

 

Qassem Soleimani (kushoto) akiwa na Abu Mahdi al-Muhandes

Kikao cha dharura cha leo Jumapili kimefanyika kutokana na maombi ya mara kwa mara yanayotolewa na wananchi wa Iraq ya kupasishwa sheria ambayo itawalazimisha askari wa Marekani kuondoka nchini humo hasa kufuatia hatua yao ya hivi karibuni ya kutumia ardhi ya nchi hiyo kutekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na naibu mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq, al-Hashdu as-Sha'abi.

Luteni Shahidi Qassim Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran SEPAH na Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq al-Hashdu as-Sha'abi wakiwa na wanzao wengine wanane waliuawa shahidi Ijumaa alfahiri katika shambulio la anga lililotekelezwa na askari gaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.

Tags