"Kutowajibishwa Israel kumeifanya iendelee kukiuka sheria za kimataifa"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73650-kutowajibishwa_israel_kumeifanya_iendelee_kukiuka_sheria_za_kimataifa
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema kutoubebesha dhima utawala haramu wa Israel kumeushajiisha na kuupa uthubutu wa kuendelea kukanyaga sheria za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2021 08:23 UTC

Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema kutoubebesha dhima utawala haramu wa Israel kumeushajiisha na kuupa uthubutu wa kuendelea kukanyaga sheria za kimataifa.

Riyadh Mansour amesema hayo katika barua aliyowaandikia António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, T. S. Tirumurti, Rais wa kiduru wa Baraza la Usalama la UN na mwenzake wa Baraza Kuu la umoja huo, Volkan Bozkir, ambapo amegusia jinai za kutisha za Tel Aviv dhidi ya Wapalestina hususan wakazi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mwanadiplomasia huyo wa Palestina UN ameashiria jinai iliyofanywa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwaua shahidi vijana wanne wa Kipalestina katika eneo la Jenin na kusisitiza kuwa, kitendo cha  wanajeshi wa Israel kuchukua maiti mbili kati ya nne za vijana Wapalestina waliowaua shahidi hivi karibuni si tu kinakiuka haki za binadamu, lakini pia ni uvunjaji wa sheria za kimataifa.   

Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza jana kwamba, vijana wanne wa Kipalestina wameuawa shahidi katika hujuma ya wanajeshi wa Israel kwenye kambi ya wakimbizi katika eneo la Jenin lililoko Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan.

Riyadh Mansour, Balozi wa Palestina UN

Riyadh Mansour ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama kuchukua hatua za dharura za kukomesha mauaji ya raia wa Kipalestina yanayofanywa kila leo na askari katili wa Israel.

Amesema chombo hicho kinapaswa kuwadhaminia usalama Wapalestina kwa mujibu wa sheria za kimataifa, sanjari na kutumia vizuri Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kuhakikisha wahanga wa jinai za Israel wanapata haki.