Bahrain kumvua uraia Sheikh Qassim kunaiweka US na UK njia panda
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9781-bahrain_kumvua_uraia_sheikh_qassim_kunaiweka_us_na_uk_njia_panda
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali hatua ya utawala wa Bahrain kumvua uraia msomi mashuhuri wa Kiislamu, Ayatullah Sheikh Isa Qassim na kusema kuwa kitendo hicho kimeziweka Marekani na Uingereza katika njia panda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2016 03:27 UTC
  • Bahrain kumvua uraia Sheikh Qassim kunaiweka US na UK njia panda

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali hatua ya utawala wa Bahrain kumvua uraia msomi mashuhuri wa Kiislamu, Ayatullah Sheikh Isa Qassim na kusema kuwa kitendo hicho kimeziweka Marekani na Uingereza katika njia panda.

Joe Stork, Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo katika eneo la Mashariki ya Kati amesema serikali za Washington na London zinafaa kujitokeza hadharani na kulaani kitendo hicho licha ya kuwa Bahrain ni muitafaki wao katika eneo hili. Ameongeza kuwa, hatua hiyo mbali na kuwa imekiuka sheria za kimataifa, lakini pia imefunga kabisa milango ya kufanyika mageuzi ya kisiasa katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Hii ni katika hali ambayo, hatua hiyo ya serikali ya Manama imeendelea kulaaniwa na asasi mbalimbali duniani, shakhsia mashuhuri na jamii ya kimataifa kwa ujumla. Tayari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Mataifa zimetoa taarifa za kulaani hatua hiyo na kusema kuwa imechukuliwa kwa jazba na kwamba inakiuka Hati ya Kimataifa ya Haki za Binadamu inayolinda haki ya uraia. Utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal-Khalifa wa Bahrain Jumatatu iliyopita ulitangaza kumvua uraia mwanazuoni mkubwa na mashuhuri wa Kiislamu nchini humo Ayatullah Isa Qasim kwa madai kuwa ametumia vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.