Mwanamke mweusi mjamzito auawa kwa kupigwa risasi na askari polisi Marekani
Polisi katika jimbo la Ohio nchini Marekani wametoa taswira ya filamu ya kamera zinazovaliwa na askari polisi inayoonyesha mwanamke mweusi mjamzito aitwaye Ta’Kiya Young akipigwa risasi, jambo ambalo limeibua taharuki na hasira ya umma huku kukitolewa wito mpya wa kukomeshwa ukatili mbaya unaofanywa na polisi wa nchi hiyo.
Mkuu wa Polisi wa Mji wa Blendon John Belford ametaja tukio hilo kama "janga" lililotokea wakati polisi walipojaribu kumzuia Young baada ya kutuhumiwa kuwa aliiba dukani.
Lakini familia ya Young imeyaelezea mauaji hayo kuwa "yanayoweza kuepukika", ya "matumizi mabaya na makubwa ya nguvu na mamlaka" na "kitendo kilichotokana na chuki".
Famila hiyo ya mwanamke huyo mjamzito imeendelea kueleza katika taarifa kama ilivyoripotiwa kama ilivyoripotiwa na gazeti la Columbus Dispatch kwamba, tukio lake linavuka kiwango cha ukiukaji wa wazi zaidi wa uchukuaji hatua kisheria. "Baada ya kuona picha za video za kifo chake, hiki ni kitendo cha uhalifu", imeongezea taarifa hiyo.
Ufyatuaji risasi huo ulitokea wakati polisi walipojaribu kusimamisha gari ya Young baada ya kutuhumiwa kuwa aliiba dukani.