Mar 28, 2024 10:09 UTC
  • Wataalamu wa US: Mapigano ya Al-Shifa yanaonyesha wapiganaji Wapalestina wangali wako imara

Wataalamu wa masuala ya vita wa Marekani wamesema, wapiganaji wa Kipalestina wamefanya mashambulizi yapatayo 70 dhidi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel karibu na hospitali ya al-Shifa katika mji wa Ghaza tangu Machi 18 wakati jeshi la utawala huo ghasibu liliporejea katika eneo hilo.

Taasisi ya Utafiti wa Vita, Institute for the Study of War  (ISW) na ile ya Mradi wa Vitisho Muhimu, Critical Threats Project (CTP) zimesema katika tathmini yao ya hivi punde kuhusiana na yanayojiri kwenye medani ya mapigano katika Ukanda wa Ghaza kwamba, kiwango hicho cha juu cha mashambulizi kinaonyesha kuwa, wanamuqawama wa Palestina wana kiwango kikubwa cha ufanisi wa mapigano katika eneo hilo, licha ya kuendelea 'juhudi' za jeshi la Israel za kulisafisha kijeshi eneo la karibu ya mji wa Ghaza.

Jopo hilo la taasisi za wataalamu wa masuala ya kijeshi zenye makao yao makuu nchini Marekani limesema, makundi yapatayo sita ya wanamuqawama wa Palestina yanapambana hivi sasa na wanajeshi wa jeshi la utawala wa Kizayuni waliotumwa karibu na hospitali ya al-Shifa.

Ripoti ya jopo hilo imebainisha kuwa, licha ya Israel kukamilisha "operesheni ya usafishaji" katika kitongoji cha Zeitoun katika mji wa Gaza mnamo Machi 3, vikosi vya jeshi la utawala huo vilirejea katika eneo hilo siku ya Jumatano, hatua inayodhihirisha kuwa wapiganaji wa Kipalestina wangali wanaendelea kuendesha harakati za kijeshi katika eneo hilo kama wanavyofanya katika maeneo mengine ya Jiji la Ghaza.

Wakati huohuo, huku vita vya mauaji ya kimbari ya jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza vikiwa vimeshasababisha hadi sasa Wapalestina zaidi ya 32,400 kuuawa shahidi wakiwemo watoto wasiopungua 15,000, makundi ya Muqawama ya Palestina na katika eneo zima la Asia Magharibi yanaendeleza operesheni zao dhidi ya utawala wa Tel Aviv na waungaji mkono wake wa Magharibi.

Kwa mujibu wa televisheni ya Press TV, katika kipindi cha saa 24 zilizopita Brigedi za Al-Qassam, Al-Quds, Mashahidi wa Al-Aqsa na Mujahideen ndani ya Ukanda wa Ghaza na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Muqawama wa Kiislamu nchini Iraq nje ya eneo hilo zimetekeleza operesheni kadhaa dhidi ya vikosi vya jeshi la Kizayuni na ngome zaidi ndani ya Ghaza na maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu yaliyopandikizwa jina bandia la Israel.../ 

Tags