Zaidi ya 44 wauawa katika mapigano Kashmir inayodhibitiwa na India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i11587-zaidi_ya_44_wauawa_katika_mapigano_kashmir_inayodhibitiwa_na_india
Zaidi ya watu 44 wameuawa kufikia Jumanne katika mapigano yalianza Julai 9 katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2016 23:23 UTC
  • Zaidi ya 44 wauawa katika mapigano Kashmir inayodhibitiwa na India

Zaidi ya watu 44 wameuawa kufikia Jumanne katika mapigano yalianza Julai 9 katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India.

Aidha watu wengine 3,500 wamejeruhiwa, wengi wakiwa na majeraha ya macho, kutokana na risasi hatari lakini zisizozua zinazotumiwa na jeshi la India kuwakandamiza waandamanaji.

Mapigano ya sasa yalianza baada ya Wani, kiongozi mwandamizi wa chama cha kupigania uhuru wa Kashmir, Hizb ul Mujahideen, kuuawa akiwa na watu wengine wawili baada ya kufyatuliana risasi na wanajeshi wa India katika eneo la Kokernag mnamo Julai 9.

Mauaji yake yaliibua ghasia katika mji wa Anantanag, ambapo maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakitoa nara za kutaka uhuru. Wanajeshi wa India wametumia risasi hai, gesi ya kutoa machozi na risasi za plasitiki zisizoua kuwatawanya waandamanaji.

Askari wa India katika eneo la Kashmir

 

Mkuu wa Polisi ya India huko Kashmir, K. Rajendra Kumar amesema kuuawa, Wani ni mafanikio makubwa katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kashmir. Aidha amejigamba kuwa polisi wameua wanamgambo 83 huko Kashmir mwaka huu pekee.

Kashmir ni jimbo lenye Waislamu wengi India na limekuwa lilikumbwa na mzozo tokea India ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947. Eneo lingine la Kashmir liko Pakistan ambayo pia ilikuwa koloni la Uingereza.  

Wakati huo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa wito wa kuwepo utulivu baina ya pande hasimu katika Kashmir inayodhibitiwa na India. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassem amesema mzozo wa Kashmir unaweza kutatuliwa kwa njia za amani na mazungumzo.